Sergio Ramos: Mshambuliaji wa Liverpool Mohamed Salah anafaa kujilaumu mwenyewe, alianza kunishika mkono
Sergio Ramos aliwaongoza Real Madrid kushinda Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya mara ya nne katika miaka mitano
Nahodha wa Real Madrid Sergio Ramos amesema hatua ya Mohamed Salah kumshika mkono kwanza ndiyo iliyosababisha mchezaji huyo wa Liverpool kuumia wakati wa fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.
Salah, 25, aliondoka uwanjani akitokwa na machozi baada ya kuumia begani.
Mchezaji huyo baadaye alifanyiwa upasuaji.
Mhispania Ramos pia aligongana na kipa wa Liverpool Loris Karius ambaye inadaiwa alipata jeraha kwenye ubongo kabla yake kufanya makosa mawili yaliyochangia Real kufunga.
Real Madrid walilaza Liverpool 3-1 kwenye mechi hiyo iliyochezewa Kiev, Ukraine.
"Kitu pekee sijasikia ni Roberto Firmino akisema kwamba alipata mafua kwa sababu aliangukiwa na jasho langu," amesema Ramos kwa kutania.
Ramos pia amedai kwamba Salah angeendelea kucheza mechi hiyo "iwapo angedungwa sindano kipindi cha pili".
Ramos, 32, ameambia AS: "Upuuzi mtupu, wamemwangazia Salah sana. Sikutaka kuzungumza kwa sababu kila kitu kimeongezwa chumvi."
"Nautazama mchezo vyema, anaushika mkono wangu kwanza na ninaanguka upande mmoja, na jeraha lilitokea kwenye mkono ule mwingine na wanasema kwamba nilishika mkono na kuukatalia kama mchezaji wa judo. Baada ya hapo, kipa wao anasema nilimduwaza kwa kumgonga.
"Niliwasiliana na Salah kupitia ujumbe, alikuwa vyema. Angeendelea kucheza iwapo angedungwa sindano kipindi cha pili. Nimefanya hivyo mara kadha lakini wakati ni Ramos alifanyajambo kama hilo, linakwamilia zaidi.
"Sijui kama ni kwa sababu umekuwa (nimekuwa) Madrid kwa muda mrefu na umeshinda kwa muda mrefu sana kiasi kwmaba watu hulitazama tofauti."
Salah alianguka vibaya na kuumia kwenye bega wakati wa kipindi cha kwanza dhidi ya Real.
Licha ya kuumia, ametajwa kwenye kikosi cha Misri kitakachocheza Kombe la Dunia nchini Urusi.
Inaaminika kwamba ingawa huenda asichezee Misri mechi yake za kwanza Urusi, huenda akashiriki mechi za baadaye.
Wengi wa mashabiki wa Liverpool wanamlaumu Ramos kutokana na kuumia kwa Salah, tukio ambalo mwamuzi hakutoa adhabu yooyte.
Ombi limeanzishwa kuwataka Fifa na Uefa kumwadhibu mchezaji huyo wa Uhispania.
Kipa Loris Karius
Wakili mmoja nchini Misri amewasilisha kesi ya kutaka Ramos atakiwe kulipa fidia ya £874m kwa madhara na hasara aliyowasababishia raia wa Misri "kimwili na kiakili."
Makosa mawili ya Karius yaliwasaidia Real kushinda na madaktari Marekani wamesema huenda kugongana kwake na Ramos kuliathiri uchezaji wake.