Abbas Tarimba, Mwenyekiti wa Kamati Maalum iliyoundwa jana na Bodi ya wadhamini ya klabu ya Yanga kusimamia masuala ya mikataba ya wachezaji pamoja na usajili, amesema wanaanza kazi mara moja.
Tarimba aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, amesema tayari wamepewa taarifa muhimu kuhusu mikataba ya wchezaji na masuala ya usajili.
Tarimba amesema kazi yao ya kwanza ni kuhakikisha wanawasainisha mikataba wachezaji wote wanaoendelea kuitumikia Yanga baada ya kutaarifiwa kuwa ni wachezaji saba tu wenye mikataba.
"Tumetaarifiwa kuwa wachezaji 7 tu ndio wana mikataba na klabu kwa sasa. Jukumu la kamati yetu kwanza kabisa ni kurudisha heshima ya Yanga nchini pia kuifanya timu ya ushindani kimataifa.
"Tutakutana haraka kuona nini kifanyike ili kuipa nguvu timu. Nguvu ya timu ni ubora wa wachezaji na benchi la ufundi kwa matokeo chanya.
"Si kazi ndogo lakini tutahakikisha tunafanya kile tunachoweza kwa dhamana yetu tuliyopewa na wanachama na Mungu atasaidia," amesema Tarimba.
Kuundwa kwa Kamati hiyo kumefufua matumaini ya kuirejeshea Yanga makali yake kwani imesheheni watu wenye mapenzi makubwa kwa klabu ya Yanga.
Tarimba ambaye ni Mwenyekiti, anasaidiwa aliyewahi kuwa Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Said Mecky Sadiq.
Kamati hiyo pia inamjumuisha Abdallah Binkleb, 'mbabe' wa masuala ya usajili.
Miaka ya nyuma Binkleb ndiye aliyekamilisha usajili wa Mbuyi Twitte aliyetua Yanga siku moja baada ya kutambulishwa na Simba kuwa wamemsajili!
Pia Kamati hiyo ina wajumbe kama Ridhiwani Kikwete, mtoto wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Mrisho Kikwete ambaye pia amewahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya usajili ya Yanga.
Wajumbe wengine ni pamoja na Hussein Nyika ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Hussein Ndanda 'Ndama mtoto wa n'gombe', Samwel Lukumay, Mashauri Lucas, Yusuphed Mhandeni, Hamad Islam, Makaga Yanga na Majid Suleiman.