Gabriel Jesus, Neymar na Philippe
Coutinho walifunga na kuwasaida Brazil kulaza Austria 3-0 mechi yao ya
mwisho ya kujiandaa kwa Kombe la Dunia mjini Vienna.
Mshambuliaji
wa Manchester City Jesus alimbwaga kipa Heinz Lindner kwa kombora la
kujipinda na kufungua ukurasa wa mabao dakika ya 35.Neymar, aliyekuwa ameanza mechi kwa mara ya kwanza tangu aumie Februari, aliongeza la pili katikati ya kipindi cha pili, baada ya kucheza kwa ubunifu mkubwa dakika ya 63.
Kiungo wa kati wa Barcelona Coutinho aliongeza la tatu muda mfupi baadaye kunako dakika ya 69.
Alifanikiwa kuukimbilia mpira uliokuwa umepenyezwa eneo la hatari na mwenzake wa zamani katika klabu ya Liverpool Roberto Firmino kabla ya kufunga.
Mambo yangekuwa mabaya zaidi kwa Austria, kwani Coutinho alitikiza mwamba wa goli dakika ya 76 naye Firmino akazuiwa kufunga na ustadi wa kipa dakika za mwisho mwisho.
Austria, walioshindwa kufuzu kwa michuano hiyo inayoanza Urusi baadaye wiki hii hawajacheza Kombe la Dunia tangu 1998.
Katika mechi hiyo, hawakutoa ushindani mkali sana kwa Brazil, ingawa mshambuliaji wa West Ham Marko Arnautovic alikaribia kufunga kipindi cha kwanza.
Brazil hawajashindwa hata mechi moja tangu Juni 2017, mechi 10.
Aidha, hawajafungwa katika mechi 16 kati ya mechi 21 walizocheza tangu kocha wao Tite alipochukua mikoba Juni 2016.
Mabingwa hao mara tano wa dunia wamepangwa Kundi E kwenye michuano hiyo na wataanza kampeni yao dhidi ya Uswizi Jumapili 17 Juni kabla ya kukutana na Costa Rica na Serbia.
Tags
KOMBE LA DUNIA 2018