Mwanasoka Bora Kati ya Okwi, Bocco, Nyoni Kujulikana Leo


KITENDAWILI cha nani anaibuka mshindi wa tuzo ya Mwanasoka Bora wa msimu uliomalizika kwa 2017/18 kinatarajiwa kuteguliwa katika sherehe maalumu itakayofanyika leo kwenye Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Tofauti na misimu iliyopita, mwaka huu tuzo hiyo inawaniwa na wachezaji wote kutoka kwa kikosi cha mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba ambao ni Mganda, Emmanuel Okwi, Erasto Nyoni na nahodha, John Bocco.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo, alisema jana kuwa mshindi wa tuzo hiyo atapatikana kutokana na idadi ya kura nyingi zilizopigwa na kwa kuwashirikisha Wahariri wa Habari za Michezo, manahodha na makocha wa timu zilizoshiriki ligi hiyo.

Ndimbo alisema pia kamati ya tuzo hizo imekamilisha uteuzi wa wachezaji watakaowania tuzo katika 'kategori' nyingine mbalimbali ambao nao washindi watajulikana leo usiku.

"Tuzo 16 zinatarajiwa kutolewa kesho (leo) usiku, ila baadhi ni za kikanuni za Ligi Kuu Tanzania Bara, ambazo tayari washindi wake wamefahamika, ambazo ni bingwa, mshindi wa pili, mshindi wa tatu, mshindi wa nne na mfungaji bora.Ukiacha hizo tano za kikanuni, zipo tuzo 10 ambazo zimefanyiwa kazi na Kamati ya Tuzo kulingana na takwimu mbalimbali za ligi hiyo, ambapo tuzo moja nyingine ya Mchezaji Bora chini ya umri wa miaka 20 (Tuzo ya Ismail Khalfan)," alisema Ndimbo.

Alizitaja tuzo nyingine zitakazotolewa siku hiyo ni ya timu yenye Nidhamu inayowaniwa na Kagera Sugar, Simba na Mtibwa Sugar, wakati Mchezaji Bora Chipukizi inawaniwa na Shaaban Idd Chilunda, Yahya Zayd (Azam) na Habibu Kiyombo (Mbao).

Mwamuzi Msaidizi Bora inawaniwa na Helen Mduma, Mohammed Mkono na Ferdinand Chacha, wakati Mwamuzi Bora wateule ni Elly Sasii, Jonesia Rukyaa na Hans Mabena wakati ile ya Kipa Bora inawaniwa ni Aron Kalambo (Prisons), Aishi Manula (Simba) na Razack Abalora (Azam).

Katika upande wa Kocha Bora, wanaochuana ni Abdallah Mohamed wa Prisons, Zuberi Katwila (Mtibwa) na Pierre Lechantre wa Simba huku Goli Bora ni Seif Karihe (Lipuli) na Shaaban Idd Chilunda wa Azam 

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post