KOCHA YANGA AWAONDOA KINA TSHISHIMBI DAR


Mwinyi Zahera

KOCHA Mkuu wa Yanga mwenye uraia wa DR Congo, Mwinyi Zahera, ameomba kambi ya nje ya Jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kujiandaa na mechi dhidi ya Gor Mahia ya nchini Kenya.

Yanga inatarajiwa kuvaana na Gor Mahia katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayopigwa Julai 17, mwaka huu, huko Kenya.

Timu hiyo hivi karibuni ilitangaza kujiondoa kwenye michuano ya Kombe la Kagame inayotarajiwa kuanza Juni 29, mwaka huu ili kupisha maandalizi ya mechi dhidi ya Gor Mahia.

Akizungumza na Championi Jumatano, Meneja Mkuu wa timu hiyo, Hafidh Saleh, alisema wachezaji na benchi la ufundi lote wanatarajiwa kuripoti siku moja kabla ya kuanza mazoezi ambayo ni Juni 24, mwaka huu kwa ajili ya kujiandaa na mchezo huo.

Saleh alisema, wakati timu hiyo ikipanga kuanza mazoezi hayo, kocha huyo tayari ametoa mapendekezo ya kambi ya nje ya Dar huku ukitajwa Mkoa wa Morogoro ndiyo uliopendekezwa.

“Baada ya mapumziko ya wiki mbili kwa wachezaji na benchi la ufundi, timu imepanga kuanza mazoezi, Juni 25, mwaka huu wakati wachezaji wakitarajiwa kuripoti siku moja kabla ya kuanza mazoezi.

“Baada ya wachezaji kuanza mazoezi haraka timu itakwenda kuweka kambi ya pamoja nje ya Dar baada ya kocha kutoa mapendekezo ya kambi ya nje ya Dar na kikubwa anataka sehemu tulivu ya mazoezi.

“Kikubwa kocha hataki kupoteza mechi hii ya Gor Mahia ili kuhakikisha tunajiweka katika nafasi ya kushinda na kujiwekea mazingira mazuri ya kufuzu katika hatua inayofuata ya michuano ya kimataifa,” alisema Saleh.

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post