Zitto aipa Yanga mchongo kutatua matatizo


Zitto Kabwe amesema kwa faida na maendeleo ya soka la Tanzania Yanga wanatakiwa kujitathmini na kuangalia changamoto zinazowakabili kuhakikisha wanakaa sawa kabla ya kuanza kwa msimu ujao.

Zitto ambaye ni shabiki kindakindaki wa ‘mnyama’ Simba amesema Yanga ni sehemu ya kukuza soka la Tanzania hivyo anaamini kamati ya mpito itafanyabkazi yake na kumaliza changamoto zinazoikabili klabu hiyo ili iweze kurudi na kushiriki michuano mbalimbali msimu ujao kama Yanga iliyozoeleka.

“Yanga walikuwa na tatizo la uongozi, tunafahamu aliyekuwa mwenyekiti wao alipata matatizo kwa hiyo wametetereka kidogo kutokana na hayo.”

“Kinachotakiwa ni wanachama, mashabiki na wapenzi wa Yanga kutafakari namna ya kutoka kwa sababu ukiwa na Yanga legelege huwezi kupata mpira mzuri hapa nyumbani, raha ya mpira ni ushindani na sisi Simba tunataka kushindana na timu bora ambayo imeimarika.”

“Mimi nawaombea heri wenzetu wa Yanga, ni jambo la kukaa chini kutafakari na kuweza kuona ni namna gani wanatatua changamoto zilizowakuta. Kama ni Manji kurudi au watafute  mtu mwingine au watu wengine wa kusaidia klabu yao iende vizuri sio lazima awe mtu mmoja.”

“Kuna haja kubwa sana ya kuangalia mifumo ya uendeshaji, mimi naunga mkono mifumo ya kiuwekezaji lakini uwekezaji wenye tija. Yanga wanatakiwa kuangalia jambo hilo na nimesikia wameunda kamati ambayo itakuja na majawabu ya changamoto zao tunawatakia kila la heri na tunahitaji Yanga imara kuweza kuwa na mpira wa ushindani.”

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post