COUTINHO AWAITA MEZANI YANGA SC


Klabu ya Al Naser ya nchini Libya, Andrey Coutinho.

KIUNGO mshambuliaji wa zamani wa Yanga hivi sasa anaichezea Klabu ya Al Naser ya nchini Libya, Andrey Coutinho amewaambia viongozi wa timu hiyo kuwa yupo tayari kurejea Jangwani muda wowote.

Coutinho, mwenye uraia wa Brazil, aliondoka Yanga msimu wa 2014/2015 baada ya timu hiyo kuusitisha mkataba wake wa miaka miwili na kurejea nyumbani kwao.

Mbrazili huyo alisajiliwa na aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Marcio Maximo ambaye alikuja pamoja na kiungo mkabaji, Emerson Oliveira kutoka nchini humo kwa ajili ya kujiunga na Yanga kabla ya kutemwa.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Coutinho alisema hana tatizo na Yanga, yupo tayari kurejea kuichezea timu hiyo kama wakimfuata na kufikia muafaka mzuri.

Coutihno alisema, Yanga ni kati ya klabu kubwa alizowahi kuzichezea kwa mapenzi yake yote, hivyo haoni sababu ya kushindwa kurejea tena Jangwani.

“Muda na wakati wowote ninawakaribisha Yanga kunifuata kwa ajili ya mazungumzo ya kuichezea timu hiyo ambayo niliwahi kuichezea kwa mafanikio makubwa ikiwemo kuchukua Ngao ya Jamii na ubingwa wa ligi kuu.

“Nakumbuka kipindi hicho ninaichezea Yanga nilikuwa bado mdogo kwa maana ya kukomaa kwa ajili ya ligi, lakini hivi sasa nimekomaa hivyo nipo tayari kurejea tena Yanga.

“Uzuri wa ligi ninaifahamu vizuri kiukweli ni ligi yenye ushindani mkubwa ambao natamani nije kucheza tena huko na timu ambayo ningependa kuichezea ni Yanga pekee na siyo nyingine,” alisema Coutinho mwenye uwezo wa kupiga mipira ya faulo.

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post