Ni ukweli usiofichika watanzania wengi walikuwa wanaumia kumuona Himid Mao anaendelea kucheza Tanzania ukilinganisha na uwezo wake, wengi waliamini Himid ni miongoni mwa wachezaji wanaostahili kucheza nje ya nchi.
‘Subira huvuta heri’ hatimaye yametimia, Himid amejiunga na Petrojet inayoshiriki ligi kuu ya Misri. Nidhamu ndani na nje ya uwanja, upambanaji na kujituma kwa 100% vina fanya watu wengi kuamini Himid atafika mbali zaidi ya alipo sasa.
Himid ni kijana asiyekubali kushindwa na hajawahi kukata tamaa, February 2017 niliwahi kufanya naye mahojiano akasimulia mambo mengi ikiwa ni pamoja na kufukuzwa shule kwa kukosa ada wakati huo alikuwa form one lakini baadaye mama yake alipambana mambo yakaenda sawa.
Huenda kumbukumbu kama hizi ndiyo zinamfanya jamaa kuwa mpambanaji tunayemuona leo ili watoto wake wasijekupita kwenye nyayo zake.
Safari hii story ya Himid si ya kusikitisha tena wala kuhuzunisha bali imejaa matumaini na malengo ya kutimiza ndoto zake kwenye soka na maisha.
Kama ulikuwa hufahamu, Himid amesaini mkataba wa miaka mitatu na klabu ya Petrojet ambayo imeanzishwa miaka 18 iliyopita. “Nimesaini miaka mitatu kucheza hapa.”
Inawezekana kabisa hata wewe ukawa unajiuliza kama mimi, kwa nini amekubali kusajiliwa na klabu changa ya Misri na Afrika kwa ujumla? Hakuna jambo ambalo limefanyika kwa bahati mbaya katika usajili wake. “Ilikuwa ndoto yenye plan ndani yake.”
“Kwanza nilitaka kuondoka Tanzania, wakati ligi inakaribia kuisha kulikua na offer kama tano za nje na tukawa na mazungumzo na timu zote ila Petrojet wakawa faster zaidi so sikuona sababu ya kuacha kujiunga nao ukizingatia level ya mpira wa Misri ipo juu sana na timu pia sio mbaya nikaona ni sehemu nzuri kwa sasa kuanzia maisha yangu nje ya Tanzania.”
Himid ameaema kwa muda mfupi ambao amekuwa Petrojet na Misri, ameshuhudia tofauti kubwa ya maendeleo ya soka ukilinganisha na Tanzania.
“Malengo yangu katika msimu wa kwanza ni kuhakikisha nacheza na kupata nafasi ya kudumu first team na kuisaidia timu kutimiza malengo yake ya msimu.”
Mara nyingi wachezaji wa Tanzania wanapopata nafasi ya kucheza kwenye nchi ambazo hazizungumzi Kiswahili wala Kiingereza changamoto kubwa huwa ni lugha, Himid yupo Misri nchi inayozungumza sana Kiarabu hali ikoje kwake?
“Changamoto ya lugha sio kubwa sana asilimia kubwa benchi la ufundi wanajua Kiingereza, kocha mkuu na madaktari wawili wanaju pia na staff baadhi wanajua Kiingereza.”
“Wachezaji baadhi wanajua Kiingereza kwa hiyo lugha sio tatizo, kwakuwa mpira una lugha yake kokote pale duniani.”
Kwa siku chache ambazo Himid amekaa Misri ameonekana kwenye picha akiwa kwenye vivutio maarufu vya utalii nchini humo (Pyramids) sehemu hiyo ilikuwa inamvutia tangu akiwa Bongo na alitamani siku moja kwenda kutembelea?
Tags
Michezo