Gor Mahia yaizima ndoto ya Simba kucheza na Everton


Kwa  mara ya pili mfululizo, Gor Mahia ya Kenya imebeba taji la SportPesa Super Cup baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Simba SC ya Dar es Salaam, Tanzania.
Mashujaa wa Gor Mahia leo wameendelea kuwa wanasoka wa kimataifa wa Rwanda, Meddie Kagere na Jaqcues Tuyisenge waliofunga mabao hayo, moja kila kipindi na kurudia mafanikio ya mwaka jana mjini Dar es Salaam wakiwafunga mahasimu wao wa Kenya, AFC Leopard 2-1 na kutwaa taji hilo.
Kagere alianza kufunga bao zuri dakika ya sita akimalizia kazi nzuri ya George Odhiambo ‘Blackberry’ kabla ya Tuyisenge kufunga la pili akimalizia krosi ya Humphrey Mieno dakika ya 54.
Simba SC ilicheza ovyo kipindi cha kwanza na kuzidiwa kabisa na Gor Mahia, lakini kipindi cha pili ilibadilika na kutulia kujaribu kucheza soka ya maelewano, ingawa tayari wapinzani wao walikuwa wamekwishajipanga kuulinda ushindi wao.
Kwa ushindi huo, Gor Mahia inayofundishwa na kocha wa zamani wa Simba, Muingereza Dylan Kerr pamoja na kuzawadiwa dola za Kimarekani 30,000 lakini watakwenda kucheza na klabu ya Everton Uwanja wa Goodison Park mjini Liverpool, England.
Simba SC watajipatia dola za Kimarekani 10,000, Singida United waliomaliza nafasi ya tatu kwa kuifunga Kakamega Homeboyz kwa penalty 5-1 baada ya sare ya 1-1 watapatiwa dola 7, 500 na wa washindi wa nne watapewa dola 5,000.
Kariobangi Sharks ya Kenya, Yanga ya Tanzania Bara na JKU ya Zanzibar kila moja itapata dola 2,500 baada ya kutolewa hatua ya kwanza ya mashindano.

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post