Na: DANIEL S.FUTE
ALIYEKUWA mchezaji wa zamani wa Barcelona Eric Abidal, anatarajia kuchukua nafasi ya kuwa mkurugenzi wa michezo katika klabu ya Barcelona kwa msimu wa 2018-19. Klabu hiyo imethibitisha kwamba, Abidal atachukua nafasi ya Robert Fernandez ambaye alikuwa akiitumikia nafasi hiyo.
Mkataba wa Robert upo mbioni kumalizika mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu, na Barcelona wamesema kwamba hawatashawishika tena katika nafasi ya kumuongezea mkataba.
Mkurugenzi huyo wa michezo anayemaliza muda wake alikabiliwa na upinzani juu ya kuondoka kwa Neymar mwaka jana katika uhamisho wa rekodi ya duniani akielekea Paris Saint-Germain. Wakati huo huo inasemekana kwamba Mkurugenzi huyu sajili zake nyingi hazikuwa za matarajio kwa klabu ya Barcelona.
Abidal aliwahi kuichezea klabu ya Barcelona katika miaka ya 2007 hadi 2013, ingawa baadae alikumbwa na ugonjwa mkubwa katika Ini lake, ambapo ilimbidi kufanyiwa upasuaji.
“Barcelona inatangaza kwamba Robert Fernandez hataweza kuongeza mkataba wake kama katibu wa timu ya kiufundi.
“Klabu hiyo inapenda kumshukuru Robert Fernandez kwa nia ya kujitolea kwake wakati ambapo yupo na Barcelona kwa miaka mingi.” alisema mwandishi kutoka La Liga.
Abidal ataanza rasmi kazi yake kama mkurugenzi mpya wa michezo ya Barcelona hapo Julai 18.