YANGA KUFANYA USAJILI WA KISHINDO MSIMU HUU




Kikosi cha Yanga kimeamua kufanya kitu kikubwa msimu huu ambapo wanaibuka na staili ya kisasa katika usajili wao mpya na kuendelea.
Mpango wa Yanga sasa ni kuhakikisha wanawasajili wachezaji ambao wanajua viwango vyao na si kuwaleta kwa ajili ya majaribio.
Usajili kama huo Yanga waliufanya walipomleta, Mcongo Papy Tshishimbi kutoka Mbambane Swallow ya Swaziland ambapo walimtuma aliyekuwa kocha wa kikosi hicho, Mzambia George Lwandamina.
Pia, walifanya hivyo kwenye usajili wa Mzimbabwe Donaldo Ngoma kutoka FC Platinum ya nchini humo akacheza kwa mafanikio kabla ya kuanza kusumbuliwa na majeraha.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika amesema kwa sasa hawatafanya zoezi la kujaribu wachezaji na wanarudisha akili waliyoitumia kumpata Tshishimbi.
"Tumetafakari na kuona hawa wachezaji wanaoletwa hapa kufanyiwa majaribio wengi wao tumekuwa tunashindwa kukubaliana na viwango vyao, wengi ni wachezaji wa kawaida  ambao klabu yetu haiwahitaji," amesema Nyika.
"Kwa sasa tunaangalia mechi mbalimbali za mashindano ya CAF tutakuwa tunafuatilia wachezaji mbalimbali kama tutaona kuna wanaotuvutia tutafanya kama ambavyo tulifanya tukawapata Ngoma na Tshishimbi ambao hata mashabiki na wanachama wetu waliwakubali."
Yanga mabingwa wa ligi kuu mara 27, wameshindwa kutamba msimu huu wa ligi kuu na sasa wanahaha kuipata nafasi ya pili wanagowania na Azam FC.
Kwa sasa kazi hiyo ya usajili itafanywa na Kocha Mkuu Mwinyi Zahera akisaidiana na benchi lake la ufundi.

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post