SIMBA YAMLETA KATONGO WA ZAMBIA MSIMUU UJAO



Image result for katongo

MTAKOMA kuringa. Ndivyo mashabiki wa Simba wanavyojisemea kimoyomoyo kupeleka ujumbe kwa watani zao Yanga. Hii ni baada ya kusikia kitu anachotaka kukifanya Kocha Mkuu wao, Pierre Lechantre.
Ni hivi. Mfaransa huyo kwa sasa anasubiri tu muafaka wake wa kubaki Simba msimu ujao ili aanze mipango yake ya usajili ambapo tayari ameshaiandaa akipanga kufanya usajili wa aina mbili ule wa wachezaji ghali kutoka timu kubwa Afrika na kutoka hapa hapa nchini. Jeuri hiyo ya Lechantre inatokana na fuko nono la fedha linalotarajiwa kutolewa na Mwekezaji wa klabu hiyo, Bilionea Mohammed ‘Mo’ Dewji.
Lechantre anayewindwa na timu ya Taifa ya Cameroon anasubiri tu, mechi ya mwisho ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Majimaji itakayopigwa keshokutwa Jumatatu mjini Songea, kabla ya kuondoka hapa nchini kwenda likizo kwao, atakuwa ameshajua hatma yake ya kubaki Simba au ndio ataondoka moja kwa moja.
Mwanaspoti limefanya mazungumzo maalumu na Lechantre na kugundua majina mawili ya mastraika ambao tayari ameshawaandika katika ripoti yake aliyoikabidhi kwa mabosi wa Msimbazi iwapo atasalia klabuni kwa msimu ujao.
Moja ya majina yaliyopo mezani mwa mabosi hao wa Simba ni la straika mkongwe na nahodha wa zamani wa Zambia, Christopher Katongo, anayeichezea Green Buffaloes.
Katongo aliiongoza Chipolopolo mwaka 2012 kubebea taji la Afrika katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) wakiizidi akili Ivory Coast, huku yeye akichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa michuano hiyo.
Mbali Ya Katongo, pia Lechantre anataka mshambuliaji mwingine mkali mzawa ili aungane na Katongo pamoja na wakali wa msimu huu; Emmanuel Okwi na John Bocco kwa nia ya kuifanya Simba itishe zaidi anga za Kimataifa na Ligi Kuu Bara msimu ujao.
“Japo huwa sipendi kumweka wazi mchezaji ninayetaka kumsajili mpaka nitakapokuwa nimemalizana naye kwa kuogopa umakini wa timu nyingine kuanza kumfuatilia, lakini miongoni mwa ninaowapigia hesabu ni Katongo,” alisema Lechantre.
“Katongo ana uwezo wa kufunga kama ilivyo kwa Okwi na Bocco, lakini yupo vizuri katika kutengeneza nafasi ana uwezo wa kushindana na mabeki wazuri Afrika na hata kupiga chenga na nina imani tukimpata ataongeza nguvu katika safu yetu ya shambuliaji,” alisema.
“Nitatengeneza timu ambayo itashindana katika mashindano ya kimataifa ambako tunatakiwa kuwa na wachezaji waliokamilika kama Katongo, naamini akishirikiana na Okwi na Bocco Simba tutafanya vizuri katika ligi na mashindano mengine.”
Mbali ya mipango hiyo, Mwanaspoti linafahamu kuwa viongozi wa Simba chini ya MO Dewji wanakuna vichwa na wapo katika vikao vizito vya ndani kwa ndani ili kuamua wanamuongezea mkataba Lechantre au wanaachana naye.
MFAHAMU KATONGO
Katongo aliyezaliwa Agosti 31, 1982 mjini Mufulira nchini Zambia, ana urefu wa futi 5 na inchi 8 na alianza kutamba akiwa na klabu ya Butondo West Tiger kabla ya kutua Kaululishi Modern Stars.
Klabu yake ya sasa inayomilikiwa na Jeshi la Zambia, Green Buffaloes ilimpaisha alipojiunga nayo mwaa 2001 na kudumu nayo hadi 2004 akiichezea mechi 75 na kuifungia mabao 20 kabla ya kutimkia zake Jomo Cosmo ya Afrika Kusini.
Jomo Cosmo alijiunga nayo 2004-2007 akiichezea mechi 72 na kuifungia mabao 36 kisha kutimka Denmark kujiunga na klabu ya Brondby kabla ya kuhamia Arminia Bielefeld ya Ujeruman na baadaye kwenda Ugiriki kuichezea Skoda Xanthi.
Mwaka 2011-13 alikuwa China akiichezeea Henna Construction kabla ya kurejea nyumbani kujiunga na Golden Arrows kwa kumda mfupi kisha kutimka tena Afrika Kusini kuichezea Bidvest Wits hadi 2015 aliporejea tena nyumbani kuichezea Buffaloes.
Mchezaji Bora huyo wa Afrika kupitia BBC- 2012 alianza kuichezea timu ya taifa ya Zambia mwaka 2003 hadi 2016 ambapo moja ya mafanikio ni kubeba taji hilo la Afrika akiwa kama nahodha, huku rekodi zinaonyesha kuwa ameichezea timu hiyo mechi 105 na kuifungia mabao 23.
Ni mahiri kwa kuwakimbiza mabeki, kumiliki mpira na kufumua mashuti kwa miguu yote mbali ya kutengeneza nafasi. Japo umri umeanza kumtupa mkono, bado anatesa ligi ya kwao.

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post