KIPA WA LIVERPOOL (KARIUS) ASHAURIWA AHAME LIVER.


Loris Karius alifanya makosa mawili kwenye fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya

Mlinda lango wa Liverpool Loris Karius ameshauriwa ahamie taifa jingine kucheza soka baada ya makosa mawili kuchangia klabu hiyo kufungwa magoli mawili katika fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya Jumamosi.

Mjerumani huyo mwenye miaka 24 analaumiwa kwa kuwasaidia Real Madrid kushinda 3-1 kwenye fainali hiyo iliyochezewa mjini Kiev, Ukraine.

Karius alitokwa na machozi baada ya kipenga cha mwisho kupulizwa huku akionekana mwenye masikitiko makubwa.

Baadaye aliwaomba radhi wachezaji wenzake, wakufunzi na mashabiki.

Kipa wa zamani wa England Robert Green ambaye mwenyewe aliwahi kufanya makosa kama hayo anasema: "Iwapo atarudi Ujerumani, ni kweli watu hawawezi kusahau alichokifanya lakini hataangaziwa zaidi."

"Kutoangaziwa sana kunaweza kuwa jambo zuri, kwenye ligi ya nyumbani, kwenda nje ya nchi ambapo watu hawakuwa wanajishughulisha sana na mechi hiyo."

Kosa la Green wakati wa Kombe la Dunia mwaka 2010 lilimfanya kufungwa bao rahisi na kusababisha mechi yao dhidi ya Marekani kumalizika 1-1.

Anasema tukio kama hilo linaweza kuwa ngumu sana kwa mlinda lango yeyote yule.

"nakumbuka baada ya Kombe la Dunia 2010 na mechi yangu ya kwanza ugenini Ligi ya Premia, kila nilipougusa mpira kulikuwa na watu kama 30,000 hivi uwanjani walikuwa wanapiga mbinja," anasema Green ambaye alichezea Norwich, West Ham, QPR na Leeds.

"Bahati mbaya kwa Karius ni kwamba nusu ya mechi ligini Uingereza ni za ugenini na anapokuwa upande wa mashabiki wageni hata uwanja wa Liverpool atakuwa anachekwa hata zaidi kama ugenini. Kipindi hiki cha kabla ya msimu kitakuwa kigumu sana kwake bila shaka.

"Makosa hutokea wakati wowote, yanaangazia zaidi unapokuwa mlinda lango ... lakini ukweli ni kwamba makosa yake yaliwagharimu ushindi mechi hiyo. Hilo litamkwamilia kwa muda lakini muhimu ni jinsi atakavyolipokea na natumai kwamba yeye kama binadamu na kipa ataweza kujikwamua na kurudi akiwa imara zaidi.

Mjerumani huyo alimpa mshambuliaji wa Real Madrid Karim Benzema bao rahisi la kwanza mjini Kiev.

Baadaye, alimruhusu Gareth Bale kufunga bao la tatu la Real kutoka mbali alipojaribu kuzuia kombora lake lakini likapita mikono yake na kutumbukia wavuni.

Hilo liliwawezesha Real kushinda taji la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kwa mara ya tatu mtawalia.

Loris Karius alihamia Liverpool kutoka Mainz ya Ujerumani kwa £4.7m Mei 2016

Karius mwenyewe alisema "anaomba radhi bila kipimo" baada ya makosa yake, kwenye ujumbe aliousambaza kwenye mitandao ya kijamii.

"Najua kwamba nilikosea sana kwa makosa yangu hayo mawili na niliwavunja moyo nyote," aliandika kwenye mitandao ya kijamii.

"Kusema kweli, sijapata usingizi hadi sasa," aliandika baada ya mechi.

"Yaliyotokea bado yanapitia kichwani mwangu tena na tena.

"Nawaomba radhi bila kipimo wachezaji wenzangu, nanyi mashabiki, na kwa wafanyakazi wote wa klabu.

"Ningelipenda sana kusongeza nyuma mshale wa saa lakini hilo haliwezekani.

"Inauma zaidi kwani sote tulihisi kwamba tungewalaza Real Madrid na tulikuwa tunacheza vyema kwa muda mrefu.

"nawashukuru sana mashabiki waliofika Kiev na kuniunga mkono, hata baada ya mechi.

"Sitalisahau hilo na kwa mara nyingine tena lilinionyesha jinsi tulivyo kama familia moja kubwa. Asanteni, na tutaerejea tukiwa na nguvu zaidi."

'Itamchukua miezi mitatu hivi kusahau'

Mwnaasaikolojia wa michezo Dkt Steve Peters, ambaye amewahi kufanya kazi na timu ya taifa ya England anasema Karius atahitaji muda kuyasahau makosa yake.

"Hii ni michezo na siku moja mambo wakati mwingine huenda mrama. Jambo muhimu zaidi ni kukubali kwamba hajapoteza kipaji chochote au uwezo wowote. Ni makosa kadha tu, kwa hivyo vyema zaidi huwa kukubali ukweli. Huenda asiwahi kurudia makosa hayo tena.

"Kwa kawaida, itamchukua miezi kama mitatu hivi kwake kukubali kwamba hayo yalipita. Hatujui ni kwa sababu gani huchukua muda kama huo - akili huchukua muda kutafakari na kulikubali jambo. Kwa usaidizi wa wataalamu, hili linaweza kufanikiwa hivi kwamba mwishowe unatokea ukiwa hata na nguvu zaidi badala ya kukudhoofisha."

Kipa wa zamani wa Ray Clemence, aliyeshinda Kombe la Ulaya akiwa na Liverpool kati ya 1977 na 1981, anasema kipindi cha mapumziko ya majira ya joto kitakuwa kirefu sana kwa Karius ambaye hakutajwa kikosi cha Kombe la Dunia cha Ujerumani.

"Alifanya makosa mawili makubwa wakati muhimu kwenye mechi na itamulazimu kuishi na hilo maisha yake yote," kipa huyo wa zamani wa England Clemence aliambia BBC Radio 5.

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post