KICHUYA AKABIDHIWA JEZI YA DONALD NGOMA YANGA


 HII inaweza kuwa habari mbaya kwa mashabiki wa Simba, baada ya watani zao wa jadi, Yanga, kuitangaza jezi namba 11 iliyoachwa na Donald Ngoma, kwamba ametengewa winga mwenye kipaji cha hali ya juu, Shiza Kichuya.

Yanga wameshaachana na straika wao, Ngoma na tayari ametangazwa rasmi kama mchezaji halali wa Azam FC, na sasa Wanajangwani hao wanafanya vikao mchana na usiku kuhakikisha Kichuya anakuwa mbadala wa Mzimbabwe huyo.

Mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wameshaambiwa kwamba winga huyo ameshamaliza mkataba wake na Simba, hivyo yupo huru kuichezea timu yoyote na sasa wanafanya kila linalowezekana kumvuta upande wa pili.

Kigogo mmoja wa Yanga ameliambia DIMBA kuwa, wakati huu ambao wapinzani wao wanadhani hawana fedha ndio wanaotaka kuutumia kufanya maangamizi ya kutisha na kama mambo yao yakienda sawa, mashabiki wao watafurahi wenyewe.

“Unajua watu wamekariri kwamba sisi hatuna fedha, lakini wanasahau kuwa Yanga ni timu yenye watu wazito ambao wanaweza wakaamua jambo na likafanyika mara moja, mimi nawaambia hamtaamini kitakachotokea.

“Msimu huu tumefanya vibaya sana, sasa hatuwezi kukubali tena msimu ujao tukaendelea kuwa mteremko, ndiyo maana tunatuliza akili zetu kuhakikisha tunafanya usajili uliotulia na huyo Kichuya ni moja ya ‘tageti’ zetu, yeye ndiye atakayepewa jezi namba 11 kama mbadala wa Ngoma endapo tutamalizana,” alisema kigogo huyo.

Kigogo huyo ameendelea kudai kuwa, mbali na Kichuya, wanatarajia kufanya usajili wa kutingisha nchi, kwani hata bilionea wao aliyeamua kuachia ngazi kutokana na matatizo binafsi yaliyokuwa yanamkabili, ameonyesha nia ya kurejea tena kuokoa jahazi.

“Nakuambia hata zile safari za kwenda kuweka kambi Uturuki zitaanza upya, kwani bosi wetu ameonyesha kila dalili ya kurejea tena, nadhani msimu ujao tutakuwa naye kama mambo yakienda vizuri, nikuhakikishie kuwa Yanga ya msimu ujao mtaomba poo,” alisema.

DIMBA liliamua kumtafuta meneja wa mchezaji huyo, Profesa Madundo Mtambo, ili kujua hatima ya mteja wake baada ya kumaliza mkataba wake na Simba na taarifa za kutakiwa Yanga ambaye alidai kuwa, mpaka sasa hajapokea ofa yoyote, lakini yupo tayari kuzungumza na timu inayomtaka.

“Ni kweli amemaliza mkataba katika Klabu ya Simba na tupo tayari kupokea ofa kutoka timu yoyote. Hizi taarifa kwamba Yanga wamezungumza na sisi ni uongo, ila tunawakaribisha mezani ili tuone ofa yao ikoje kwa sababu hii ni biashara kama biashara nyingine,” alisema.

Kwa upande wake Kaimu rais wa Simba, Abdallah Salim ‘Try Again,’ alikiri mchezaji wao kumaliza mkataba na kudai muda wowote watakaa meza moja na kijana wao ili kuzungumzia mkataba mpya.

“Kichuya ni mchezaji muhimu kwenye timu yetu, hivyo tunasubiri tu muda ufike tumsainishe mkataba mpya baada ya huu wa awali kumalizika, tumeishi naye vizuri na amekuwa na mchango mkubwa kwetu, ndiyo maana hatutaki kumpoteza,” alisema.

DIMBA lilimtafuta Mwenyekiti wa Usajili wa Yanga ambaye ndiye anatajwa kufanya mchakato wa kuhakikishia Kichuya anakuwa mali yao, Husein Nyika, lakini simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post