#2DaysToKiev, nani ana ulinzi salama na nani ana ushambuliaji kiwembe Liverpool vs Madrid?
Tunaendelea na habari na makala za kuelekea fainali ya michuano ya Champions League pale Kiev siku ya Jumamosi, baada ya kuona ubora wa Milner sasa tutizame maeneo mawili muhimu ya Ulinzi na Ushambuliaji kwa timu hizi mbili kwa kile walichofanya msimu huu.
ULINZI.
Suala la ulinzi ni gumzo haswa, watu wanasema Liverpool wana safu mbovu ya ulinzi kuliko Real Madrid, na wengi wanaamini Real Madrid wako katika ulinzi salama kuliko Liverpool, lakini ukweli ni upi?
Katika michezo 12 ya Champions ya Real Madrid msimu huu, Madrid wana clean sheets 3 tu katika mechi hizo, na hii ina maana katika michezo 9 ya Los Blancos waliruhusu nyavu zao kutikiswa.
Msimu wa 2016/2017 Real Madrid walifungwa mabao 17 katika Champions League, msimu huu wameshafungwa 15. Tangu msimu wa 2003/2004 hakuna timu ambayo ilienda hadi fainali huku ikiwa imefungwa mabao kuanzia 15, hili tu linatosha kufahamu hali ya ulinzi ya Real Madrid.
Liverpool wenyewe hadi sasa wameshatobolewa mara 13 huku 6 ikiwa katika mchezo mmoja wa nusu fainali vs As Roma ikiwa ni mabao 2 pungufu na Real Madrid, lakini katika clean sheets majogoo hawa wa London hawajafungwa katika mechi 6 ikiwa ni 3 zaidi ya Real Madrid.
Lakini Liverpool wanaonekana wamekuwa wakipoteana kadri dakika zinavyokwenda ,takwimu zinaonesha Liverpool katika mechi 5 zilizopita za CL dakika 12 za mwanzo waliongoza kwa mabao 12-3, lakini dakika 15 za mwisho walipoteza kwa 6-1 katika mechi hizo.
USHAMBULIAJI.
Kwa miaka sasa BBC(Benzema, Bale na Cristiano) imekuwa ikizungumziwa kama utatu hatari zaidi duniani wakifuatiwa na MSN(Messi, Suarez na Neymar). Msimu wa 2013/2014 BBC walifunga mabao 28 kwa ujumla(Bale 6, Ronaldo 17 na Benzema 5) wakiivunja rekodi ya MSN ya mabao 27 mwaka 2014/2015.
Lakini msimu huu habari ni tofauti kabisa, hakuna strike force hatari katika Champions League kama utatu wa Mane, Salah na Firminho na hadi sasa wameshaivunja rekodi ya BBC ya 2013/2014 ya mabao 28 kwani hafi sasa Salah ana 10, Firminho 10 na Mane 10.
Msimu huu Liverpool ndio klabu inaongoza kwa mabao Champions League, mabao 40. Ni Barcelona 1999/2000(42) na Real Madrid 2014/2015(41) ndio klabu pekee ambazo zimewahi kufunga mabao mengi zaidi ya Liverpool katika historia ya michuano hiyo.
Lakini pamoja na hayo yupo Cristiano Ronaldo ambaye hadi sasa ana mabao 15 katika Champions League(mabao 5 zaidi kuliko vinara wa ufungaji wa Liverpool), Ronaldo anahitaji mabao 2 kuifikia rekodi yake mwenyewe ya mabao 17 mwaka 2014/2015 na ana njaa katika fainali hii kwani akibeba kombe atakuwa nyota wa kwanza kubeba CL 3 mfululizo.