Maandalizi ya Harusi ya Alikiba Kufulu Tupu ...... Mapambo tu Zaidi ya Milioni 40


Wakati zikiwa zimesalia saa chache kabla mwanamuziki Alikiba hajafunga ndoa jijini Mombasa, imebainika kuwa ametumia mamilioni katika maandalizi ya sherehe hiyo. 

Mwandishi wetu aliyepo Mombasa, Mohammed Ahmed anaripoti kuwa mapambo katika ukumbi utakaofanyika sherehe hiyo yamegharimu Sh2 milioni za Kenya ambazo ni wastani wa Sh40 milioni za Tanzania. 

Mpambaji wa ukumbi wa Diamond Jubilee unaochukua watu 1,500 katika jiji hilo ambaye mwandishi wetu alimkuta akiendelea na kazi,  anasema amelipwa kiasi hicho cha fedha ambacho ni kikubwa kulingana na aina ya mapambo waliochagua maharusi. 

Alikiba anayetamba na wimbo Seduce Me anatarajia kufunga ndoa kesho na mrembo Amina ambaye anatokea Mtaa wa Kongowea katika jiji hilo. 

Inaelezwa kuwa familia ya binti huyo ina uhusiano wa karibu na Gavana wa Mombasa, Hassan Joho ambaye ni rafiki wa Alikiba. 

Inaaminika kuwa Joho ndio amesaidia kwa kiasi kikubwa kumuunganisha Kiba na familia ya Amina, ambapo safari zake za mara kwa mara mjini Mombasa, hazikuwa kwa shughuli za kimuziki tu bali ni kuwa karibu na mkewe huyo mtarajiwa. 

Harusi hiyo inatarajiwa kurushwa mubashara kwenye runinga ya Azam kuanzia Mombasa ambako Joho na vigogo wengine wa Muungano wa NASA wanatarajiwa kuhudhuria huku sherehe ya hapa nchini, Tanzania Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete anatajwa kuwa miongoni mwa wageni waalikwa

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post