Cristiano Ronaldo
alifunga mojawapo ya mabao bora zaidi katika Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya
kwa bao la kushangaza la 'bicycle-kick' na kuwasaidia Real Madrid
kuwalawa Juventus katika mechi ya mkondo wa kwanza ya robofainali.
Ronaldo aliandika historia kwa mabao yote mawili.Kwanza, alifikia krosi ya Isco na kufunga bao la Real la kwanza dakika ya 3 ambapo aliweka historia kwa kuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao katika mechi 10 mtawalia Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.
Juve walikuwa na nafasi ya kusawazisha kipindi cha kwanza ingawa Toni Kroos alikaribia pia kufunga kwa kombora kali lililogonga mwamba wa goli. Alipiga kiki hiyo akiwa hatua 25 kutoka kwenye goli.
Kisha, wakati wa 'mfalme' wa soka kutoka Ureno ukawadia.
Dani Carvajal alituma krosi eneo la hatari na Ronaldo akapaa juu angani na kutoa kiki kali ambayo ilimwacha kipa stadi wa Juve Gianluigi Buffon akiwa ameduwaa dakika ya 64.
Bao hilo lilikuwa la ustadi mkubwa kiasi kwamba mashabiki wa Juventus ya Italia, ambao bila shaka walivunjiwa matumaini ya kufika nusufainali na bao hilo, walisimama na kumshangilia Ronaldo.
Waitaliano hao walijipata wakitumbukia kwenye taabu zaidi baada ya Paulo Dybala kuoneshwa kadi ya pili ya manjano na kufukuzwa uwanjani dakika ya 66 kwa kumchezea visivyo Carvajal.
Marcelo alikamilisha ushindi dakika ya 72 kwa kucheza moja mbili na Ronaldo kabla ya kufunga.
Meneja wa Real Madrid Zinedine Zidane alivyolipokea bao hilo la pili la Ronaldo ilitosha kufahamu ustadi uliotumiwa.
Alitingisha kichwa chake na kuonekana kupigwa na butwaa usoni, alipindua kichwa upande na kisha kuonekana kulikubali.
Katika maisha yake ya uchezaji alifunga mabao mengi ya kushangaza akiwa Turin mwenyewe, lakini alichokiona kutoka kwa Cristiano Ronaldo kilikuwa cha kipekee.
Ronaldo, 33, alikuwa ameruka juu kana kwamba ni kawaida yake tu na kuutuma mpira kimiani.
Baada ya mpira kutulia kwenye wavu, mashabiki wa Juve walimfuata Zidane na kusimama kumshangilia Ronaldo.
Winga wa zamani wa Scotland ambaye alikuwa akitangazia BBC Radio 5 live alishangazwa pia na Ronaldo.
"Unapoona mpira unaelekea kwake, unafikiria 'Oh, hautajaribu kuupiga mpira huyo kwa kuupitisha juu cha kichwa chako.' Kisha, pa! Unajionea mwenyewe, unatazama."
"Si jambo la kawaida. Watu wanazungumzia jinsi Ronaldo anazeeka sasa - lakini hakuna kasoro yoyote kwenye mwili wake iwapo anaweza kufanya jambo kama hilo. Alipima vyema kabisa, na ubunifu wa kufanya hivyo ni wa kushangaza."
Ufungaji mabao wa Ronaldo
- Ronaldo amefunga mabao 19 mechi zake tisa za karibuni zaidi akichezea Real - 25 mechi 13 alizochezea nchi yake na klabu karibuni zaidi
- Amefunga mabao 39 mechi 36 alizochezea Real msimu huu - mabao mengi kushinda mchezaji mwingine yeyote yule anayecheza ligi tano kuu za Ulaya (England, Ufaransa, Ujerumani, Italia na Uhispania)
- Amefunga mabao katika mechi 10 alizocheza karibuni zaidi Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya mtawalia - tisa msimu huu na wakati wa fainali msimu uliopita - kwa jumla amefunga mabao 16
- Ronaldo ndiye mfungaji mabao bora Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya akiwa na mabao 119 - mabao 19 mbele ya Lionel Messi wa Barcelona.
- Amefunga mabao tisa kati ya makombora yake 11 yaliyolenga lango dhidi ya kipa maarufu Gianluigi Buffon.
- Ronaldo amekuwa akifungia Real Madrid bao la kwanza mechi za Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya katika mechi 10 kati ya 14 walizocheza karibuni zaidi
- Amefunga mabao 22 robofainali Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, moja zaidi ya Juventus. Ni timu tano pekee, ikiwemo Real Madrid, ambazo zimefunga zaidi ya hapo hatua hiyo.
- Ronaldo amefunga (14) au kusaidia ufungaji (mara tatu) 68% wa mabao yote 25 ya Real Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu huu
- Amefunga katika kila mechi sita alizocheza dhidi ya Juventus - mabao tisa kwa jumla. Hakuna mchezaji aliyefunga mabao zaidi dhidi ya timu moja Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kuliko yeye.
"Bila shaka watu wanazungumzia bao hilo la pili, lilikuwa zuri ajabu, pengine bao bora zaidi nililowahi kufunga," Ronaldo alisema baada ya mechi.
"Lilikuwa la kuvutia sana. Niliruka juu sana na ni bao ambalo litakumbukwa muda mrefu.
"Nimekuwa nikisubiri kufanya hivyo kwa muda mrefu, lakini hutegemea na hali ya mechi. Ilinijia tu kwamba nijaribu, lazima daima ujaribu. Nilijaribu na nikafanikiwa."
Akizungumzia kuhusu kupongezwa na mashabiki wote uwanjani, alisema ni jambo la kipekee.
"Nilikwua mdogo, niliwapenda Juventus na hali kwamba mashabiki walio walinishangilia itasalia daima akilini mwangu."
Walichosema wengine
Kipa wa Juventus Gianluigi Buffon: "Ronaldo ni bingwa wa kipekee. Kwa pamoja na Lionel Messi, ndiye peke yake ambaye hukoleza ushindi muhimu wa timu yake, na anafaa kulinganishwa na [Diego] Maradona na Pele."Beki wa Juve Andrea Barzagli: "Cristiano aliliunda vyema bao hilo la pili. Ni kama bao la Playstation."
Kocha wa Juventus Massimiliano Allegri: "Sikui kama bao hilo la Cristiano ndilo bora zaidi katika historia ya soka, lakini lilikuwa la kipekee. Unaweza tu kumpongeza kwa yale anayoyafanya kwa sasa."
Meneja wa Real Madrid Zinedine Zidane: "Cristiano Ronaldo ni tofauti. Ni mchezaji tofauti na wengine na daima ana hamu ya kufanya jambo la kipekee Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya. Huwa hapumziki na kuleweshwa na sifa anazopokea."
"Bao hilo lilikuwa la kipekee, ingawa alikuwa amepoteza nafasi nyingine mbili rahisi zaidi. Ndivyo soka ilivyo."
Zlatan Ibrahmovic anayechezea LA Galaxy kwa sasa, ambaye alifunga bao la kushangaza kutoka hatua 30 ndani uwanjani dhidi ya England mwaka 2012 alisema: "Lilikuwa bao zuri, lakini pengine anafaa kujaribu kutoka mita 40."
'Bao langu lilikuwa bora...'
Meneja wake Zinedine Zidane huenda alifurahishwa sana an bao la Ronaldo, lakini ana mtazamo tofauti.
Alifunga bao moja la kushangaza pia Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kwenye fainali ya 2002 akichezea Real dhidi ya Bayer Leverkusen.
Kwake, bao gani lilikuwa bora zaidi?
"Oh langu! Bila shaka ni langu."
Tags
MICHEZO KIMATAIFA