JK Ajitosa Kumpeleka India Mzee Mjuto kwa Matibabu


LICHA ya kufanyiwa upasuaji wa tezi dume bado hali ya staa wa filamu za Kibongo, Amri Athuman ‘Mzee Majuto’ ni tete ambapo Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Mrisho Kikwete ‘JK’, amejitosa baada ya kumuona alivyodhoofu kwa sasa.

JK na Mzee Majuto walikutana uso kwa uso wikiendi iliyopita katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar ambako kulikuwa na shughuli ya utoaji tuzo za filamu zilizojulikana kwa jina la Tuzo za Kimataifa za Sinema Zetu ambapo walionekana wakiteta kwa dakika kadhaa kabla ya kila mmoja akaenda kukaa kwenye siti yake.

Mzee Majuto alionekana akiwa amedhoofu kwani aliingia ukumbini akitembea kwa msaada wa fimbo huku akionekana kutokuwa mchangamfu kama ilivyo kawaida yake, hali iliyowahuzunisha mashabiki wake waliokuwa ukumbini hapo.

Risasi Mchanganyiko lilizungumza na Mzee Majuto ili kujua hali yake na kile alichokuwa akiteta na JK ambapo alisema kuwa, kutokana na hali yake kutokuwa nzuri licha ya kufanyiwa upasuaji, rais huyo alimuahidi kwamba watajadili na watampeleka India kwa matibabu zaidi kwani tiba za hapa hajaridhishwa nazo.

 “JK ameniahidi kwamba watanipeleka India kwa ajili ya matibabu ikiwa ni baada ya kwenda na kujadili na rais aliyeko madarakani Dk John Pombe Magufuli ‘JPM’ ili nikapate matibabu zaidi maana tiba nilizopatiwa hapa bado sijakaa sawa.

“Kwanza kwa sasa nimepatwa ugonjwa mpya tena ambapo mkono unaniuma mno, ninashindwa hata kushika chochote ndiyo nataka nirudi tena hospitalini nikawaeleze kuhusu hilo maana hali siyo nzuri kabisa,” alisema Mzee Majuto.

Hata hivyo, Mzee Majuto alisema kuwa, pamoja na hilo, JK alimuahidi kwamba atamnunulia trekta kwa ajili ya kulima kwenye mashamba yake ambako atapanda minazi huko Tanga ili aweze kuendesha maisha.

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post