Ngumu kumeza iliyogusa, wachezaji, mawakala, usajili


Wakala wa mwanamichezo anatambulika kisheria kama mwakilishi wa kocha, mchezaji, kwenye mikataba ya michezo baina ya mchezaji na timu au  mwanamichezo na taasisi nyingine akisimamia haki za msingi pamoja na faida za mwakilishi wake kibiashara.

Wakala kwenye michezo ni rafiki wa mchezaji, mshauri, mbunifu wa masuala ya kimaendeleo kwa wanamichezo, msimamizi wa masuala ya kibiashara na wakati mwingine anaweza kuwa msimamizi wa haki.

Kabla ya miaka ya 1990, wachezaji wengi wa mpira wa miguu walikuwa hawatumii mawakala, wachache kati yao waliwatumia zaidi baba zao kama wawakilishi. Kutokana na wazazi wengi kutokuwa na uelewa wa masuala ya biashara ya mpira wa miguu, wachezaji wengi waliibiwa haki zao na wengine walilipwa ujira mdogo kuliko kilichotakiwa kwenye mikataba yao na vilabu.

Mpaka mwaka 1995 Sweden ilikuwa na mawakala watatu tu wa mpira wa miguu lakini hadi kufikia mwaka 2002 walikuwa na mawakala 33, kwa mujibu wa Fifa mpaka sasa kuna mawakala 5187 wenye leseni dunia nzima mawakala hao Italy ikitoa mawakala 600. Mawakala hupokea fungu la asilimia 4 mpaka 10 kutokana na mikataba ya wachezaji na hupata asilimia 10 mpaka 20 kutoka kwa makampuni au taasisi zilizowekeza fedha kwa mchezaji.

Kutoka enzi zile wachezaji wanaitwa kusajiliwa pale kwenye mgahawa wa chakula cha dunia, kuchukua pesa bila kuhesabu, shuhuda za wachezaji wanaosajiliwa kwenye ligi ya Tanzania zinastaajabisha na kuacha maswali mengi kichwani. Mtu mmoja anasema, wacha waendelee kutapeliwa muda mwingine wanayataka wenyewe.

Kama asilimia 4-15 akichukua msimamizi na kwenda kichwa-kichwa kupigwa na watu wa kati si kunatofauti kubwa sana? Pamoja na mvuto mkubwa aliokuwa nao Ulimboka Mwakingwe mwanzoni mwa miaka ya 2000, alisajiliwa na klabu ya Simba kwa kupewa seti ya sofa pamoja na baiskeli ya gia, tafakari tu katika hali ya kawaida endapo angekuwa na wakala kama biashara hiyo ingewezekana.

Mtu mwingine anaibuka anasema, mpira wa Bongo una maumivu kwa watu wengi, mkataba wa Geoffrey Mwashiuya unamalizika miezi minne ijayo kwenye klabu ya Yanga, kwa kilichomkuta kwenye usajili wa kwanza aliokuwa anatoka Mbozi kuja Dar angekuwa na wakala nadhani ‘kikombe kile kingemuepuka’.

Nauliza kwani ilikuwaje mzee baba? Jamaa anasema, pamoja na Nsajigwa kumfuatilia Mwashiuya kwa zaidi ya miezi mitatu pia vilabu vingine vilikuwa vinamfuatilia, Mwashiuya alitumiwa nauli akaja Dar alipofika tu akapokelewa na akina Seif Mandinga na Bin Kleb.

Mtoto wa Kinyiha kutoka Mbozi, alizuzuka bwana alipopanda vogue kwa mara ya kwanza kitu kilichomvuruga mpaka anaulizwa tukulipe mshahara kiasi gani Mwashiuya akajibu, nilipeni laki tatu tu kwa mwezi, wawakilishi wa Yanga walishikwa na kigugumizi cha mshangao mmoja wao akasema, unasema? Mwashiuya akajibu, laki tatu tu kina Mandinga wakasema, usiwaze kijana tutakulipa laki tano kwa mwezi.

Mzee mwenzangu huwezi kuamini, kwenye usajili wa Mwashiuya waliofaidika kwenye ule usajili ni timu ya Kimondo kuliko hata mchezaji. Kimondo walipata milioni 36 kutokana na mapato yote ya mlangoni waliyoyachukua kwenye mechi dhidi ya Yanga ambayo ilichezwa Vuawa. Biashara ilikwenda namna hiyo kutokana na mchezaji kutokuwa na msimamizi yeyote sio wakala wala meneja kitu kinachopelekea haki zake zingine kama bonus na vitu vingine visijadiliwe kwenye pande mbalimbali za mkataba huo.

Mtu mmoja anasema, wachezaji lazima wakubali kuwa na wasimamizi vinginevyo watatendewa vitu vya ajabu, huwezi kuamini, kuna mchezaji mmoja wa timu kubwa tu hapa nchini alisajiliwa na ahadi aliyopewa ilikuwa ni kupelekwa hospitali kufanyiwa tohara.

Jamaa mmoja anaibuka anasema, unakumbuka hata bishara ya Ngasa kwenda Sudan ilikwama kutokana na mchezaji huyo kutokuwa na msimamizi, Ngasa angekuwa na msimamizi si dhani kama msimamizi wake angekubali mchezaji wake azime simu na kujifungia hotelini juma zima wakati fuko la pesa likiwa linamtafuta, lakini wapotoshaji walitumia nafasi ya kutokuwepo wakala kumpotosha Anko ambaye kipindi hicho hakutaka kusikia la mtu yeyote hata Chibabubabu.

Hata Buswita angekuwa na msimamizi anayejitambua kuliko Mtabora si dhani kama angeshauriwa asaini mara mbili kwenye vilabu vya Simba na Yanga kisha wajifiche kwenye utetezi wa kupitiwa na Shetani.

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post