Muamuzi wa Chelsea vs Barcelona 2009 akiri kuibeba Barca na kulazimika kuikimbia hotel usiku wa manane


Tom Hernning Ovrebo ni kati ya waamuzi ambao mashabiki wa Chelsea hawawezi kuja kumsahau, muamuzi huyu ndiyo alikuwepo uwanjani mwaka 2009 wakati wa nusu fainali kati ya Chelsea vs Barcelona.

Baada ya filimbi ya mwisho ya mchezo kupigwa mashabiki wa Chelsea walionekana kuwa na hasira zilizopita kwa muamuzi huyu na sio mashabiki tu bali hata wachezaji walionekana kutokumuelewa.

Didier Drogba uvumilivu ulimshinda kabisa na alimfuata muamuzi huyo hadi usoni kumuambia maneno mabaya(matusi), hii ilikuja baada ya muamuzi huyo kuwatosa Chelsea penati zaidi ya tatu katika dakika 90.

Baada ya mchezo huo muamuzi huyo alikiri kwamba kweli alifanya makosa katika mchezo huo ambayo yaliigharimu Chelsea kwani Barcelona walifudhu kwa bao la ugenini kwenda fainali.

Akiongea na gazeti moja nchini Hispania alisema “ni kweli nilikosea lakini nilifanya kosa ambalo binadamu yeyote anaweza kulifanya,nilifanya maamuzi mabaya na kama sio yale naamini Barcelona wangetolewa.”

Ovrebo amedai kwamba baada ya mchezo huo hakutaka hata kuongea na mchezaji yeyote alitaka kwenda tu kwenye vyumba vya kubadili nguo huku akikumbuka Michael Ballack alivyotaka kumsukuma.

Usiku nao wakati wa kulala haukuwa mzuri kwake na wasaidizi wake kwani walipokea ujumbe wa vitisho kutoka kwa baadhi ya mashabiki wa Chelsea hali ambayo ilipelekea kuhama hotel waliyofikia.

Kesho Chelsea watakuwa uwanjani kwa mara nyingine katika hatua ya 16 bora wakiikaribisha Barcelona katika mchezo ambao mashabiki wa Chelsea wanausubiria kwa hamu kwani bado wana uchungu na walichofanyiwa 2009.

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post