Yanga imesonga mbele kwenye michuano ya vilabu bingwa Afrika licha ya kutoka sare ya kufungana 1-1 ugenini dhidi ya St Louis ya Seychelles ikiwa ni mchezo wa marudiano, vigogo hao wa VPL walishinda 1-0 katika mchezo wa kwanza uliochezwa uwanja wa taifa Dar hivyo Yanga wamefuzu kwa jumla ya magoli 2-1.
Ibrahim Ajib ndiye aliyeihakikishia Yanga kusonga mbele katika hatua inayofuata baada ya kuifungia timu yake goli dakika ya 45 kipindi cha kwanza lililoifanya Yanga iongoze, dakika ya 90+1 St Louis wakasawazisha na kufanya mchezo huo kumalizika kwa sare ya 1-1.
Mara baada ya mchezo huo kumalizika, mlinzi wa kulia wa yanga Hassan ramadhani ‘kessy’ amesema, walichokifuata Seychelles na sasa wanarudi kwa ajili ya kukomaa na VPL.
“Tulichokuwa tunakitaka tumekipata kwa hiyo wanayanga waendelee kutuunga mkono wasikate tamaa kwa mechi zijazo. Tumeshatoka hatua moja tumeenda nyingine, sasa tunarudi kwenye ligi”-Ramadhani Kessy, beki Yanga.
Yanga ambayo ndio bingwa mtetezi wa taji la VPL ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 37 nyuma ya mnyama simba inayoongoza ligi kwa pointi zake 42. Yanga ikirejea nchini, mchezo wake unaofuata wa ligi ni dhidi ya Ndanda utaochezwa Nangwanda Sijaona, Mtwara.