Jacob Zuma Agoma Kujiuzulu Urais


Rais Jacob Zuma amekataa kujiuzulu mara moja kama mkuu wa nchi, wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama cha African National Congress (ANC) iliyoamua kumuita.

Uamuzi wa chombo hicho cha juu cha uamuzi cha chama kiliamua kumuita kikitumia kifungu kilichomo katika Katiba ya ANC kinachoipa halmashauri hiyo mamlaka ya kumuita mtumishi wa Serikali.

Chama kilikuwa kinatarajiwa kumuandikia Zuma barua Jumanne asubuhi kumfahamisha kuhusu uamuzi huo.

Halmashauri Kuu ilifanyika mkutano wa saa 13 mfululizo huko Irene nje kidogo ya Pretoria. Kikao hicho kilichoitishwa kwa haraka kilianza saa 8:00 Jumatatu mchana na kumalizika saa 9:00 usiku kuamkia Jumanne.

Saa 5:00 usiku NEC iliamuru kumuelekeza Rais wa ANC, Cyril Ramaphosa na Katibu mkuu, Ace Magashule kwenda nyumbani kwa Zuma kwenye makazi yake Mahlamba Ndlofu mjini Pretoria kumpa hati ya kujiuzulu au kukubali kufukuzwa na chama.

Kikao kati ya wajumbe wawili hao na Zuma kilidumu chini ya saa moja ambapo mkuu huyo wa nchi alikataa kutii.

Ramaphosa na Magashule walirudi kwenye kikao cha NEC na kutoa mrejesho saa 6:00 usiku. Ukumbi ulikuwa umefungwa wakati ambapo wale wawili waliondoka kwenda kukutana na Zuma.

Vyanzo kutoka ndani ya NEC vililiambia shirika la News24 kwamba wakati wa kikao cha watatu hao Zuma aliwauliza wajumbe waliotumwa: "Kitu gani kibaya nimefanya".

"Zuma aliwajibu Ramaphosa na Magashule kuwa atawajibu hadharani chama kitakapokuwa kimeamua kumwita," kilisema chanzo.

ANC inatarajiwa kuzungumza na vyombo vya habari juu ya matokeo ya mkutano wa NEC saa 6:00 Jumanne mchana. Zuma inasemekana anataka kuendelea kubaki kwenye majengo ya Serikali yaitwayo Umoja kwa miezi mitatu ili aweze kushiriki matukio mawili. Hata hivyo, NEC ilikataa masharti yake.

Vyanzo vilisisitiza kuwa Zuma alitaka kubaki kama mkuu wa Serikali hadi wakati wa mkutano wa kilele wa nchi nne za Brics utakapofanyika na alitaka kuhudhuria mkutano mwingine wa Umoja wa Afrika.

Mkutano wa Brics umepangwa kufanyika Julai mjini Sandton ikiwa na maana Zuma atakuwa madarakani kwa miezi mitano zaidi. Zuma aliiongoza Afrika Kusini kuingia kwenye umoja wa kiuchumi wa Brazil, Russia, India na China maarufu kama Brics.

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post