Serikali
imewaagiza wakuu wote wa vyuo vya elimu ya juu kuacha urasimu katika
utoaji wa fedha kwa wanufaika wa mikopo ambao wana makubaliano na
Serikali.
Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema leo
bungeni ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Spika Job Ndugai lililotaka
serikali kutoa kauli kuhusu wanafunzi wa mwaka wa kwanza kutakiwa kutoa
fedha ili wasajiliwe kabla ya kupata mikopo.
Agizo
la Spika lilitokana na Mwongozo uliombwa na Mbunge wa Viti Maalum (CCM)
Martha Mlata ambaye alieleza bunge kuwa wanafunzi wamekuwa wakihangaika
vyuoni baada ya kutakiwa walipe fedha za usajili kabla ya kupewa mkopo.
"Serikali
imeshawaagiza wakuu wa vyuo vya elimu ya juu kuacha urasimu katika
utoaji wa fedha kwa wanufaika kwa mikopo ambao wana makubaliano na
Serikali," amesema.
Amesema
inasikitisha sana kuona baadhi ya vyuo vinadiriki hata kuwakataa
wanafunzi waliowadahili wao wenyewe au vinawalazimisha wachukue programu
tofauti na walizokuwa wamechaguliwa awali na vyuo husika.
"
Jambo hili halikubaliki hata kidogo na linaleta shaka kuhusu uadilifu
wa vyuo husika. Naiagiza TCU (Tume ya Vyuo Vikuu) na Kurugenzi ya Elimu
ya Juu ya Wizara, kufuatilia kwa karibu mambo yote yanayopendelea vyuoni
wakati wanafunzi wanaripoti na kubainisha wote wanaokiuka taratibu na
kuwanyima wanafunzi haki yao ya kusoma programu wanazoitaka," amesema.
Amesema
Serikali haitasita kuchukua hatua kali kwa vyuo vyote vitakavyoleta
usumbufu usio wa lazima kwa wanafunzi na kuwafanya wapoteze muda ambao
wanapaswa kuutumia kwa masomo.
Tags
kitaifa