Rais John Magufuli amewataka wabunge wawili wa CCM, Nape Nnauye na Hussein Bashe, ambao michango yao bungeni imekosoa uendeshaji uchumi, wampelekee majina ya wawekezaji wanaokwamishwa ili awape kazi.
Wabunge hao wa Mtama na Nzega Mjini waliikosoa Serikali wakati wa kujadili Mpango wa Taifa wa Maendeleo kwa mwaka 2018/2019.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ambaye alishutumiwa na wabunge hao kumpotosha Rais, alisema wakati akihitimisha mjadala huo kuwa alipigiwa simu na mkuu wa nchi na kuelezwa hayo.
“Naomba ninong’one na Bunge lako tukufu. Mheshimiwa Rais Magufuli aliposikia huu mjadala, alinipigia simu na aliniambia hivi,” alisema Waziri Mpango.
“Waziri, mwambie ndugu yako mheshimiwa Nape na mheshimiwa Bashe kuwa nawataka sana hao wawekezaji kwenye ujenzi wa Standard Gauge Railway.
“Wawalete hata kesho niko tayari kuwapa reli ya kutoka Kaliua –Mpanda au Isaka-Mwanza au reli ya Mtwara-Mchuchuma hadi Liganga waijenge.
“Hayo ni maneno ya mheshimiwa Rais. Natumaini waheshimiwa husika will raise up to this challenge from his excellence the president (wataifanyia kazi changamoto ya mheshimiwa Rais.”
Akijibu hoja za wabunge hao na wengine, Dk Mpango alisema si kwamba Serikali imeiweka pembeni sekta binafsi bali bado haijakaa vizuri na wakati mwingine inakuja na masharti yasiyotekelezeka.
Tags
Siasa