Dr Shika Afunguka Kwa Kirefu Maisha Yake...Tazama Hii Video Mwanzo Mwisho



AKIZUNGUMZA na Global TV Online leo na matangazo hayo kurushwa  jioni hii saa 10:30, Dkt. Louis Shika ambaye amepata umaarufu mkubwa baada ya kushiriki katika mnada wa nyumba za Said Lugumi jijini Dar es Salaam na baadaye ‘kukwaruzana’ na jeshi la polisi kutokana na mchakato wa mnada huo, amefunguka engi kuhusu maisha yake.

Katika simulizi hiyo, Dkt Shika ambaye hivi sasa ni maarufu kama ‘900 Itapendeza’ kutokana na mambo yaliyojiri katika mnada huo, alianza kwa kusema kwamba neno ‘daktari’ linalotangulia jina lake ni la kitaalam, yaani kweli yeye ni daktari wa binadamu akiwa alisomea taaluma hiyo nchini Urusi.

“Nilisomea utaalam huo nchini Urusi nilikokwenda mwaka 1984 kwenda kuchukua digrii ya kwanza ya miaka saba ambayo niliimaliza mwaka 1991,” anasema daktari huyo mwenye mwili wa kiasi na kimo kirefu.

Anaendelea kusema kwamba mwaka huohuo aliamua kuunganisha masomo apate digrii ya pili ya magonjwa ya kuambukiza (infectious diseases) ambayo alimaliza mwaka 1993.

Alishindwa kuchukua digrii ya tatu (PhD) kwani sehemu alikokuwa akisomea, kusini mwa Urusi, Chechnya, palizuka vita baina ya jimbo hilo na serikali, hali iliyomlazimu kukimbilia jijini Moscow kwenda kuendelea na digrii ya tatu.
Huko alifanikisha lengo lake hilo na kuanza kufundisha katika chuo hichohicho alichokuwa akisomea hadi akapata digrii ya nne.

Wakati akiendelea na shughuli za ufundishaji, aliangua kujingiza katika ujasiriamali na hivyo kufungua kampuni aliyoipa jina la Lancefort Ltd.  Hilo lilifanyika Julai 28, 1999 alipofungua kiwanda cha zana za madawa ya kilimo na kiwandani.

Akifafanua, alisema kiwanda hicho alikinunua kutokana na kuwekeza fedha alizokuwa anazipata kwa kufundisha na zingine alizoongezwa na marafiki.
Kiwanda hicho, alisema, kilitokana na mabaki ya viwanda vilivyoshindwa kufanya kazi wakati wa Ukomunisti na hivyo serikali ikawa inaviuza kwa waliovitaka.

“Nilinunua viwanda zaidi ya kumi vya kilimo,” anasema.
Kuhusu uangalizi wa viwanda vyake vilivyoko Urusi wakati yeye akiwa hapa, Dkt. Shika alisema hilo halimpi matatizo kwani kuna watu wenye uwezo wa kuviendesha wakati yeye akiwa hapa.

Pia alimtaja kiongozi wa zamani wa Urusi, Mikhail Sergei Gorbachyov, kuwa ni mmoja wa viongozi na wasimamizi wa viwanda vyake hadi sasa, hivyo hana wasiwasi wowote akiwa huku.

Kuhusu kilichomfanya kuja nyumbani Tanzania, mzee huyo alisema  alikuja nchini Januari Mosi, 2005 baada ya kutekwa na majambazi wa Kirusi mwaka 2004 wakimataka awake  dola milioni moja na nusu za Marekani.
Akifafanua, alisema majambazi hayo yalimshikilia kwa siku 28 katika sehemu ambayo hakuifahamu baada ya kumvizia alipokuwa akikaribia nyumbani kwake na kumteka.

Mateso makubwa aliyoyapata wakati wa kutekwa huko ikiwa ni pamoja na kupigwa, kuwekewa nyaya za umeme na kadhalika, ni pamoja na kukatwa vidole viwili vya mkono wa kushoto na kimoja mkono wa kulia, vyote kwa kutumia shoka.

Pamoja na kulazimishwa aiambie benki yake itoe fedha kwa ajili yake, yote hayo hayakufanikiwa kwa vile benki walihisi kulikuwa na njama za kumshurutisha kufanya hivyo.
Hata hivyo, baada ya mateso yote hayo, alifanikiwa kutoroka kutoka sehemu hiyo majambazi wengine walipoondoka na kumuacha mwenzao ambaye alilewa pombe kali na kujidunga madawa ya kulevya.
Baada ya tukio hilo ndipo alipoamua kurejea nyumbani ambako anaendelea kuishi hadi sasa.
Simulizi hii ya kusisimua inaendelea kesho Global TV Online,hivyo usikose kuiona.

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post