Wanasayansi kutoka China watajaribu kukuza viazi kwenye Mwezi kama sehemu ya safari yao watakayoifanya hivi karibuni kwenye Mwezi.
Kwa mujibu wa taarifa katika gazeti la Chongqing Morning Post, viazi hivyo vitakuzwa ndani ya mfumo wa mazingira ambao utakuwa umedhibitiwa.
Hiyo itakuwa sehemu ya majukumu ya wana anga watakaosafiri kwa kutumia chombo cha anga za juu cha Chang'e-4 mwaka ujao.
Watakuwa kwenye chombo kimoja cha umbo la mcheduara pia na nondo wa hariri ambao pia watakuwa wanafanyiwa majaribio, Profesa Xie Gengxin wa chuo kikuu cha Chongqing aliambia gazeti hilo.
Lengo ni kuona iwapo wadudu hao na viazi hivyo vinaweza kuishi na kukua kwenye Mwezi.
Matokeo yake ni kwamba watapata habari za kina zaidi kuhusu uwezekano wa binadamu kuhamia kwenye Mwezi na kuishi huko, kituo cha redio cha China Radio International kinasema.
Viazi vilitumiwa kwenye filamu ya kuigiza ya The Martian ya mwaka 2015, ambayo iliigiza jinsi mwana anga aliyekwama sayari ya Mars alifanikiwa kuishi kwa kukuza viazi.
Matt Damon aliigiza mwana anga huyo katika filamu hiyo ilifuata hadithi ya kitabu cha Andy Weir.