KUPITIA safu hii uipendayo, leo ninakupa njia nne zitakazolifanya penzi
lako liendelee kunoga, hata kama litakuwa limeanza kufubaa utaliamsha
upya.
Wengi wamekuwa hawaelewi mambo mengi kuhusu uhusiano ndiyo maana huishia
kulalamika kwamba wanapenda sana lakini mwisho wa siku huishia
kutendwa.
Hakuna mtu ambaye hahitaji faraja, kila aliyekuwa na mpenzi wake
anahitaji kuwa na furaha. Hakuna mtu ambaye anaingia kwenye mapenzi ili
apate msongo wa mawazo, kila mtu anayediriki kuutoa moyo wake, kitu cha
kwanza anachokitarajia ni faraja kisha furaha.
Ipo hivyo! Watu wengi wanakuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi huku wakiwa
na matumaini kwamba hao waliokuwanao inawezekana watakuwa wapenzi wa
maisha yao yote. Pasipo kujua, wakati mwingine kuna makosa hufanyika,
mtu hajui afanye nini ili penzi alilonalo kwa mpenzi wake linoge, hajui
ni njia zipi zitamfanya kupendwa kila siku.
Leo nitakutajia njia chache ambazo kama utazifanya, nakuhakikishia penzi lenu litashamiri zaidi ya lilivyo hivi sasa.
MPE UHURU KWANZA
Kila mtu anapenda kuwa huru, kuachwa afanye mambo yake anayoyapenda.
Hakuna mtu anayependa kuingiliwa, hasa kwenye masuala ya kutumia simu
yake. Kama kweli unahitaji penzi linoge, usitake kuingilia mambo yake
hasa katika matumizi ya simu, unachotakiwa ni kumwambia muda ambao
hupendi kuona akizungumza na simu na si kwamba kila unapoona simu yake
inaita, unaichukua kwa nguvu.
Mapenzi hayapo hivyo, mpe uhuru mwenza wako. Haimaanishi mtu kama
hajatulia basi kuchukua simu muda wote inapoita ndiyo kutamfanya
kutulia, hapana, bali kwa kufanya hivyo utampa mbinu nyingine ya kuweza
kupambana nawe. Unachotakiwa ni kumfanya kuwa huru, usimuingilie.
CHUKUA MUDA WAKO KUMTOA ‘OUT’
Wengi hukosea hapa, huwa hawapendi kwenda matembezi na wapenzi wao.
Wengine hujifanya wapo bize, hata ukimwambia Jumamosi nataka tutoke out
atakwambia anataka kufanya hili na lile.
Rafiki yangu, kila mtu anahitaji kuwa karibu na mpenzi wake, hakuna
anayependa kuwa na mpenzi ambaye muda wote yupo bize tu. Mchukue, nenda
naye sehemu. Kutoka mitoko ya mara kwa mara itawafanya muwe karibu
zaidi, itawafanya muda wote mzidi kupendana, ila kama utajifanya upo
bize, jua kuna mtu ataitumia nafasi hiyo kutoka na umpendaye.
PENDELEA KUFANYA UTANI
Hakuna mtu anayempenda mpenzi ambaye yupo siriazi saa ishirini na nne.
Pata muda wa kukaa na kutaniana naye. Mchombeze kwa vineno vya utani,
mpetipeti, mlaze kitandani na uanze kupiganapigana naye vibao vya
kimahaba hata kwa kutumia mito ya kulalia.
Unapokuwa siriazi kila wakati inakuwa ni vigumu mwenzako kulifaidi
penzi, pendelea kutabasamu inapobidi kila unapokuwa na mpenzi wako, siyo
kila atakachokwambia wewe uso wako umekunja ndita kiasi kwamba
ataonekana kukuogopa na kumtafuta mtu mwingine ambaye atahitaji kuliona
tabasamu lake, atahitaji kuona akifanyiwa utani wa mahaba nk.
HEBU MSIFIESIFIE BASI
Wengi wanaogopa kuwasifia wapenzi wao, hawajui kama kila mtu duniani
anapenda kusifiwa. Mpenzi wako anapovaa nguo nzuri zilizomtoa, usikae
kimya, mwambie amependeza kwani hilo litamfanya kufurahi sana. Kama
utakuwa na mpenzi halafu kila siku humsifii hata akifanya kitu gani, jua
kwamba atajisikia vibaya, wakati mwingine atahisi hayupo sawa kwa kuwa
tu hujawahi kumsifia.
Unapomsifia mpenzi wako kunamfanya kuongeza umakini katika kuvaa kwake,
kununua manukato na hata jinsi atakavyosuka au kunyoa atafanya kwa ubora
wa hali ya juu kwa kuwa anajua utamsifia
Tags
Mapenzi