Ukweli Mchungu...Hili la Straika Mzungu wa Simba na Kocha Maki ni Zaidi ya Kichekesho

 


Nipo bize kidogo na mambo fulani. Wiki imekwenda kasi kwa harakati za hapa na pale. Hakuna kupumzika.

Lakini pamoja na yote bado vituko vya soka letu vinanigusa sana. Ni vituko kweli kweli. Sijui tulirogwa na nani. Ama aliyeturoga keshakufa.


Nimesikia habari nyingi kuhusu Simba. Tulia kwanza tutazijadili moja moja. Tuanze na hili la Simba kusajili straika Mserbia, Dejan Georgjivic. Huyu aliyetambulishwa na Meneja Habari wa Simba, Ahmed Ally alikaririwa akimuita katika tamasha la Simba Day; ‘Mlete Mzungu...Mlete Mzungu...!’


Ni kweli tumefikia hatua ya timu zetu kusajili nyota mzungu? Nadhani hapana. Simba imeamua kutupa kali ya mwaka.


Ubaya ni kwamba Dejan mwenyewe anaonekana ‘Wa mchongo’. Hana maajabu yoyote. Yaani ni mchezaji wa kawaida.


Sijui ni nani amemleta pale Simba. Kama ni mapendekezo ya Kocha Mkuu, Zoran Maki basi Simba walipaswa kumwambia ukweli. Nadharia zake hazifanyi kazi kwenye soka letu.


Hata kama angekuwa mchezaji mzuri, bado ni ngumu kwa mchezaji kutoka Ulaya kung’ara katika soka letu. Bado soka letu halijawa la kisasa kiasi hicho cha straika mzungu kukupa unachotaka.


Soka letu linahitaji wachezaji wagumu. Sio kama Dejan. Tumeona mastraika wengi laini laini wamekuja hapa na kushindwa kunawiri.


Hivyo kwa kifupi siyo tu kwamba sitegemei makubwa kutoka kwa Dejan, bali sitegemei chochote. Siku zake kwenye Ligi yetu zinahesabika kirahisi kama fedha za masikini.


Namuona akiachwa wakati wa dirisha dogo tu hapo. Namuona akiachwa kwa aibu. Kwanini tumefikia huku? Ni kwa sababu watu wanafanya mambo nje ya uhalisia.


Kwa akili zako yule straika Dejan anaweza kutamba kwenye viwanja vya Manungu, Mkwakwani na Sokoine? Thubutuu. Akitamba mje mnipige nimekaa palee.


Kituko zaidi ni hizi taarifa za kocha Zoran Maki kuwakataa baadhi ya wachezaji waliosajiliwa dirisha hili. Nasikia amemkataa Victor Akpan aliyesajiliwa kutoka Coastal Union.


Amesema hamudu kucheza katika nafasi ya kiungo mkabaji. Kwamba Akpan anahama sana nafasi na hana utulivu. Akpan huyu huyu? Inachekesha sana.


Yaani viongozi wa Simba wametumia zaidi Milioni 100 kumpata Akpan. Lakini ajabu kocha anakuja na kumkataa ndani ya wiki chache tu. Hapa kuna kitu hakipo sawa.


Nasikia pia amemkataa Nasoro Kapama kwa madai kuwa ana uwezo mdogo kucheza Simba. Huyu ni mchezaji ambaye alipendekezwa na kocha Pablo Franco. Viongozi wa Simba wakamalizana naye mapema.


Leo kocha mpya amekuja na kumkataa. Yawezekana kweli Kapama hana uwezo mkubwa sana. Lakini Zoran angempa muda kwanza. Angalau mpaka dirisha dogo. Tuone kweli kama hana uwezo.


Hili la kukataa wachezaji mapema kwangu naona sio sawa. Kuna wachezaji wanahitaji muda kuonyesha uwezo. Hasa mchezaji kama Kapama ambaye hajawahi kucheza timu kubwa. Unatarajia aanze kwa gia ndogo pale Simba. Lakini kocha hamtaki kabisa. Inasikitisha.


Kumbuka kwamba mapema Zoran aliwakataa Meddie Kagere, Chris Mugalu na Taddeo Lwanga kwamba hawana uwezo. Simba ikalazimika kuachana nao. Sasa wiki chache tu mbele kawakataa wengine.


Kuna namna huyu kocha anaifanya kazi yake kuwa ngumu pale Simba. Ni kweli katika eneo lake yeye ni mtaalam zaidi, lakini hili la kukataa wachezaji wengi linafikirisha. Tena sana.


Yote kwa yote Simba bado inahitaji straika mwingine wa maana wa kusaidiana na Moses Phiri. Hawa kina Habib Kyombo na Dejan sio wa kuwategemea sana. Hasa kwenye mechi za CAF. Muda utasema ukweli.

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post