NI ukweli usiopingika kuwa mwanamke ndiye mhimili mkubwa katika ujenzi wa uhusiano wowote wa kimapenzi au ndoa.
Nafasi
yake kubwa hujengwa na mambo mbalimbali kiasili katika maumbile kama
vile uvumilivu, kuwa mkweli (kwa kiasi kikubwa) na tabia njema.
Kwa
wanaotambua na kuheshimu nafasi zao kama wanawake katika ujenzi wa
penzi, wataungana nami kukubali kuwa mapungufu mengi yanayojitokeza
katika mahusiano na ndoa huchangiwa na mapungufu ya mwanamke.
Mshauri
Boston Globe anaamini kwamba nguzo imara katika ujenzi wa uhusiano
imara ni mwanamke na inapokuwa kinyume chake, ni udhaifu wa mwanamke
huyo huyo ndio husababisha.
"Mwanamke
ana nafasi ya kuongoza kinachotakiwa kufanyika penzini, busara katika
utatuzi wa matatizo na tabia za kuvutia mwanaume na jamii kwa maana ya
familia," anasema.
Aidha, pamoja na mambo
mengine, tabia zifuatazo zinatajwa kama kero ambazo ni ngumu kuvumilika
katika uhusiano na ikitokea kuharibia mambo yako, ujilaumu wewe
mwenyewe:
1. KUONGEA SANA
Kuongea ni
njia pekee ya mawasiliano na nzuri katika kuwasilisha hisia kwa mwanaume
kuhusu upendo namna unavyompenda na masuala mengine ya maisha.
Lakini
wapo wanawake wanaongea sana kama 'cherehani' kiasi cha kukera.
Mwanaume anajuta kufahamiana na wewe kwa jinsi ulivyo mjuaji na
mzungumzaji wa kila jambo bila kubagua hadhira.
Na
tafiti nyingi zimeonesha kuwa mahusiano ya kimapenzi na ndoa nyingi
hushindwa kufikia malengo kutokana na uwepo wa mwanamke anayesema tu
kila wakati.
Hali hii huzalisha uvujaji wa siri
na mipango ya ndani, lawama (zisizo na msingi), simulizi zisizo na tija
za matukio ya ndugu, jamaa na majirani hadi kufikia wakati mwingine
kusutwa kutokana na usambazaji wa maneno ovyo.
Hakuna
mwanaume makini atakayevumilia kuwa katika uhusiano na mtu wa aina hii
na unajikuta pamoja na kuwa na sifa nyingi nyinginezo, unakosa penzi
endelevu na kukimbiwa kila wakati.
2. MPENZI PESA
Pamoja
na umuhimu wa pesa katika kuendesha maisha yakiwemo masuala ya mapenzi,
wapo wanaoamini katika ujenzi wa msingi wa uhusiano katika pesa. Hili
ni tatizo.
Kipo kipande cha wimbo wa DDC
Mlimani Park, dansi kisemacho 'hata njiwa ana mpenzi wake kwenye tundu
ingawa njiwa hajui pesa wala shilingi'.
Ndio.
Maisha ni kutafuta (pesa) lakini si kwa kuuza upendo au kutumia pesa
kama fimbo ya kukuongoza kupata penzi sahihi, kwani hakuna kamwe bei ya
upendo popote pale duniani.
Inashauriwa
kutoegemea sana katika mahitaji ya pesa kutoka penzini, kwani msingi wa
uhusiano na ndoa ni upendo wa dhati na si pesa.
Chagua kuwa 'mpenzi pesa' uone namna utakavyomaliza soli za viatu vyako kutafuta mwanaume.
Unapaswa
kujiamini katika utafutaji binafsi wa maisha ili ukikutana na pesa kwa
mpenzi ziwe chachu tu ya kurahisisha maendeleo utakayoyaongoza na si
kutaka 'kuchuna buzi' tu kila wakati.
3. ULEVI KUPINDUKIA
Miongoni
mwa burudani zinazotumiwa na wengi katika muda wa kufurahi na wapenzi
ni unywaji wa pombe na wanawake wengi sana hivi sasa ni wanywaji wazuri.
Haina shida!
Lakini mshauri Ann Koleen anataja
ulevi kama sifa mojawapo mbaya sana kwa mwanamke, kwani ikizidi
hupoteza staha, jambo ambalo ni hatari sana kwa wapendanao.
Wapo
wanaotumbukia katika matukio mengi maovu bila kukusudia chanzo, kikiwa
ni pombe na mara nyingi ulevi humfanya mlevi kuanika tabia zake halisi
bila kificho jambo linalowafelisha wengi kufikia malengo yao kimapenzi.
Koleen
anasema mwanamke anapaswa kuwa mtu makini wakati wote akifanya kila
jambo kwa kiasi na ikibidi awe kiongozi wa mwanaume dhidi ya unywaji
sahihi.
"Ukiwa mlevi wa kukesha kwenye baa
huwezi kuwa mke mwema na hutapata mwanaume makini labda mlevi mwenzako..
ni hatari kushiriki mapenzi yenye msingi wa pombe," anasisitiza.
Pamoja
na madhara mengine, mwanamke mlevi atafifisha maendeleo binafsi na ya
familia kutokana na ukweli kuwa pombe, kama zilivyo starehe nyingine,
zina gharama kubwa.