NYOTA wa Klabu ya Gwambina FC, Meshack Abraham anatajwa kuzichonganisha Yanga na Simba ambazo zinatajwa kuwania saini yake ili kuongeza nguvu ndani ya vikosi vyao.
Nyota huyo ambaye anavutana shati na mzawa John Bocco anayekipiga ndani ya Simba kwenye chati ya ufungaji amefunga mabao sita huku Bocco akiwa ni namba moja na mabao yake saba.
Habari zinaeleza kuwa Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Cedric Kaze inahitaji mzawa mmoja mwenye uwezo wa kucheka na nyavu ili awe mbadala wa Michael Sarpong ambaye kasi yake ni ya kusuasua akiwa na mabao manne.
Kwa upande wa Simba wao wanahitaji mbadala wa Charlse Ilanfya ambaye mambo kwake yamekuwa magumu kwa kushindwa kuonyesha kile walichotarajia baada ya kuipata saini yake kutoka ndani ya KMC.
Akizungumza na Saleh Jembe, Mkuu wa Idara ya Mashindano ndani ya Gwambina FC, Mohamed Almas maarufu kama Mtabora amesema kuwa bado hawajapokea ofa kwa sasa wanasubiri dirisha dogo lifunguliwe kwanza.
"Kwa sasa dirisha dogo la usajili bado hivyo hakuna ofa ya mchezaji wetu Meshack, tunasubiri tuone itakuaje kama wanaweza kuja hilo ni jambo la kukaa mezani," .
Nyota mwenyewe Meshack amesema kuwa hana tatizo akipewa taarifa kuhusu kucheza katika timu hizo kwa kuwa kazi yake ni mpira.