IBRAHIM Ajibu na mshikaji wake Miraj Athuman wazawa wenye ushkaji mkubwa ndani ya benchi kwenye Ligi Kuu Bara ndani ya Klabu ya Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Sven Vandenbroeck inaelezwa kuwa wanaweza kuibukia Namungo.
Msimu wa 2020/21 umekuwa na ushindani wa namba ndani ya Simba ambao ni mabingwa watetezi huku nyota hao wakiwa miongoni mwa wahanga wa kusugua benchi.
Kwenye mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Plateau United hakuna hata mmoja aliyeweza kuyeyusha hata dakika moja ndani ya uwanja.
Hali hiyo imewafanya nyota hao kuwekwa kwenye rada za Namungo ambayo inashiriki Kombe la Shirikisho Afrika.
Kabla ya kupigwa chini kwa Kocha Mkuu, Hitimana Thiery alikuwa amependekeza jina la Ibrahim Ajibu kujiunga na klabu hiyo hivyo kwa kuwa kwa sasa ameshapigwa chini inaelezwa kuwa mabosi wa Namungo wanafikiria kumvutia kasi nyota huyo.
"Ajibu alikuwa kwenye mpango wa Namungo zama zile za Hitimana ila kwa sasa inaonekana nafasi yake ipo hivyo ni suala la kusubiri namna gani wanaweza kuwapata nyota hao ndani ya Simba.
"Pia yule Miraj,(Athuman) ni miongoni mwa nyota ambao wanapigiwa hesabu kutua Namungo hivyo mambo yakiwa sawa watakuwa na changamoto mpya nje ya Simba," ilieleza taarifa hiyo.
Mwenyekiti wa Namungo, Hassan Zidadu hivi karibuni aliweka wazi kuwa mpango mkubwa wa timu hiyo ni kuwa na wachezaji wazuri ambao watafanikisha malengo ya timu hiyo kimataifa.