“Kukaa kijiweni na kusubiri ajira za Serikali mtazamo hasi” Spika Ndugai

 

Spika wa Bunge, Job Ndugai amewataka vijana kuacha fikra potofu ya kusubiri kuajiriwa na serikali, badala yake watumie fursa zilizopo kuibua miradi mbalimbali itakayowainua kiuchumi.

Alitoa rai hiyo kwenye hafla ya uzinduzi wa ibada maalumu iliyofanyika kwenye Kanisa la Kristo Mfalme Angalikani Chamwino mkoani Dodoma juzi kwa ajili ya kuwahamasisha Watanzania kuzipenda bidhaa zinazozalishwa nchini.

“Bado kuna baadhi ya vijana wanaendelea kukaa vijiweni kusubiri nafasi za ajira serikalini suala ambalo ni mtazamo hasi, hivi sasa kuna fursa nyingi zinazoweza kuwaingizia kipato ikiwamo ufugaji, kilimo cha zao la zabibu na bustani za mboga badala kuendelea kukaa vijiweni kusubiri kuajiriwa.” Ndugai

“Inasikitisha kuona vijana hivi sasa wanashinda vijiweni na majumbani na simu zao kwa ajili ya kuchati kutafuta ajira na vitu ambavyo havina faida kwao wakati muda huo wangeweza kushughulika na akili ya kuibua miradi mbalimbali ambayo ingewatoa kwenye umaskini,” Ndugai

Aidha, Ndugai alitoa wito kwa wamiliki wa viwanda vinavyozalisha bidhaa mbalimbali nchini kuhakikisha vinakuwa na bidhaa zenye ubora ili Watanzania waendelee kujivunia na kuzipenda zaidi bidhaa zao.

“Viwanda vikizalisha bidhaa zenye ubora Watanzania watazithamini na kusaidia kukuza uchumi wa nchi na ajira kuongezeka,” Ndugai

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post