Makosa yanayofanywa na wanawake wengi katika mahusiano ya kimapenzi

 


Hakuna kitu kizuri kwenye uhusiano kama kuishi vizuri, uhusiano usiwe na ugomviugomvi wa kila mara. Kila mmoja aujue wajibu wake kwa mwenzake, amsome mwenzake ni mtu wa aina gani ili kuweza kujua namna ya kuishi naye. Mathalan ni vyema kumsoma mwenzi wako kama ni mtu wa hasira sana, ujue namna ya kuishi naye. Anapokuwa na hasira, usimueleze kosa lake au kumkosoa. Subiri hasira zitakaposhuka, mueleze katika lugha rafiki na hapo utakuwa umeepusha mengi.

Kumueleza mtu makosa yake katika wakati ambao naye ana hasira, utasababisha hasira zimpande zaidi na kusababisha hata ugomvi mkubwa hivyo busara zaidi zinapaswa kutumika. Mjue mwenzi wako ni mtu wa aina gani kisha ishi naye kwa staili unayoona inafaa. Kuna makosa mengi ambayo huwa wapendanao wanayafanya lakini katika makala haya leo nitazungumzia makosa ambayo ni hatari na yanafanywa na wanawake kwa wanaume wao.

Kung’ang’ania jambo
Mara nyingi wanaume huwa hawapendi kuona mwanamke anang’ang’ania jambo moja kwa muda mrefu. Hawapendi kuona mwanamke anashinikiza jambo kwa kiasi ambacho kinamnyima amani. Hata kama unajua upo sahihi, mwanamke unapaswa kutoonesha uking’ang’anizi kwa mwanaume wako. Mueleze mara moja jambo, mara ya pili ukiona hakuelewi muache kwanza.

Anakuwa anapima jambo lako na wakati mwingine akili yake inakubaliana na kile unachomueleza lakini namna unavyomng’ang’ania, unavyomshinikiza anaweza akajisikia vibaya. Mueleze mara moja, mara ya pili kisha wewe hamia kwenye mada nyingine. Utamkumbushia tena kesho au kesho kutwa na si lazima utake jambo hilo umueleze siku hiyo na siku hiyohiyo upate jibu la kueleweka. Anaweza asikuelewe siku hiyo lakini kesho yake ukaona mwenyewe ametekeleza katika namna fulani lile jambo ulilokuwa unamueleza.

Kujilinganisha
Hili nalo ni kosa kubwa ambalo linafanywa pia hata na wanaume lakini zaidi wanawake. Baadhi ya wanawake wana kasumba ya kupenda kujilinganisha maisha ya wenzao na kutaka wafanyiwe na wenzi wao. Hili ni kosa. Uhusiano wenu unapaswa kuwa wenu.

Msiwaige watu wanavyoishi, usijaribu kujilinganisha nao halafu ndio utake kufanana
nao, ishini maisha yenu, wekeni ndoto zenu mnazotaka kuzifikia. Mathalan unataka uwe na mapazia, makochi au rangi nzuri ya nyumba, mavazi na kadhalika, wekeni mikakati yenu na mjue namna ya kufikia mafanikio yenu. Msilaumiane kuyakosa mafanikio. Tengenezeni mfumo wa kuyafikia malengo yenu katika muda muafaka.

Ubize na marafiki
Hili nalo ni tatizo. Wapo baadhi ya wanawake ambao wanajisahau. Kipaumbele cha maisha yao wanakitoa kwa marafiki au familia na kumfanya mwanaume wake kama mtu wa ziada. Unapaswa kumpa thamani mwanaume wako kuliko mtu mwingine yeyote. Onesha jinsi unavyomheshimu, anapofika nyumbani hata kama ulikuwa na mazungumzo na marafiki au wageni wowote basi onesha kumjali mumeo. Siyo anafika wewe upo bize tu na marafiki au watoto wako. Muoneshe unamjali,
unamthamini na unampa kipaumbele maishani mwako. Ukifanya hivyo utamfanya mwanaume ajisikie yupo wenye mikono salama na atazidi kukupenda kwelikweli

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post