Baada ya Morrison…Tshishimbi Naye Simba, Apewa Mkataba Kufuru


BAADA ya kumalizana na winga wa Yanga, Mghana, Benard Morrison uongozi wa Simba umerudi kwa kasi kwa aliyekuwa nahodha na kiungo wa Yanga, Papy Tshishimbi raia wa DR Congo kwa lengo la kutaka kumsajili kwa ajili ya msimu ujao.

Simba wamefufua mazungumzo na kiungo huyo ambaye kwa sasa ni mchezaji huru baada ya kuachwa na Yanga kufuatia mkataba wake kumalizika kabla ya kutangaza kumtema. Inaelezwa Simba wamemuandalia mkataba wenye maslahi mazuri.

Licha ya kuwepo kwa taarifa nyingi za kiungo huyo lakini Championi limethibitishiwa kuwa moja ya sababu za kumtaka kiungo huyo kwa sasa ni kutokana na Mbrazil, Gerson Fraga kudaiwa kuomba kuondoka kwenye kikosi hicho.

Pia kuna madai ya usumbufu na utovu wa nidhamu wa mara kwa mara kutoka kwa kiungo mkongwe wa timu hiyo, Jonas Mkude, hivyo Papy analetwa kwa lengo la kumpa changamoto.

Kingine ni kwamba wameona hakuna haja ya kumleta mchezaji mwingine kutoka nje na Tanzania, ambaye atakuja kuanza upya, hivyo Papy amepewa nafasi kubwa kwa kuwa ni mchezaji huru, lakini pia ameshaijua ligi ya Bongo na anayafahamu vema mazingira ya soka letu.

Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba, uongozi wa timu hiyo utakamilisha mazungumzo ya kumsajili kiungo huyo wakati wowote huku wakiwa wamepanga kumpa mkataba wa miaka miwili.

“Suala la mazungumzo na Tshishimbi yapo na yanakwenda vizuri kwa sababu uongozi umedhamiria kumleta Simba na ukiangalia yule ni mchezaji huru kwa sasa baada ya kumaliza mkataba wake na Yanga.
“Mkakati uliopo ni kumpa mkataba wa miaka miwili na tayari mkataba upo, tayari umeshaandaliwa, ndiyo maana nakwambia haziwezi zikapita siku mbili atakuwa ameshatambulishwa na kuna mambo mengi ya kiufundi yameangaliwa ili timu iweze kupata faida na siyo jambo ambalo watu wamelikurupukia,” kilisema chanzo hicho.

Championi lilimtafuta kiungo huyo ili kujua ukweli wa taarifa hizo, ambapo alisema: “Mimi ni mchezaji huru kwa sasa na soka ndiyo kazi yangu, naweza kwenda kucheza popote na timu yoyote ambayo itakuwa inahitaji huduma yangu, maana mpaka sasa nina ofa za timu nyingi, fahamu tu kwamba nina ofa nyingi, naangalia ipi itakuwa na maslahi kabla ya kuamua.”

Lakini kwa upande wa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Masingiza hakuwa tayari kuongelea suala hilo huku mara kadhaa akisisitiza taarifa rasmi za timu hiyo zitatolewa na vyanzo vyao husika vya habari.

IBRAHIM MUSSA NA ISSA LIPONDA, Dar

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post