Siri ya Utajiri wa Magari na Majumba wa Harmonize Yafichuka

MARA baada ya msanii Rajabu Abdul, ‘Harmonize’ au Harmo kulamba dili la mamilioni kutoka Benki ya CRDB, baadhi ya watu ni kama walipigwa na shoti ya umeme na kubaki midomo wazi.

Kwa mapana na marefu Risasi Mchanganyiko limepata siri kwa nini msanii huyo amepata dili hilo kubwa na siyo msanii mwingine yeyote Bongo.


Akizungumza na mwandishi wetu mmoja wa mameneja wa Harmonize ajulikanaye kwa jina la Mchopa alisema: “Kilichombeba sana ni nidhamu, kujituma, kukubalika kwenye jamii, moyo wa uzalendo kwa taifa lake na ubora wa kazi zake.”

Akizungumzia mpunga aliopiga msanii huyo, Mchopa alisema kuwa, ni fedha ndefu lakini akasita kuziweka kwenye ‘figa’ kwa sababu ya kuheshimu masharti yaliyopo kwenye mkataba wao na CRDB.


Alisema, mpaka benki kubwa kama hiyo inampa mkataba Harmonize, ujue kuna utafiti wa kina umefanyika hadi kufika kwenye uamuzi huo.

“CRDB siyo benki ndogo hapa nchini, ni benki kiongozi ya wazalendo na wajasiriamali wa nchi hii.

“Ukiona wamemtambua msanii wetu, basi jua hawakumchagua kwa utamu wa jina lake bali kazi zake, hii ndiyo sifa ambayo sisi kama menejimenti tunajivunia kwa Harmonize.

“Maana kwenye nchi yetu kuna wasanii wengi tena wakubwa wenye majina makubwa, lakini hawakupata nafasi hii,” alisema Mchopa.

Wakizungumza na mwandishi wetu baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, walisema kuwa msanii huyo anafaa kuwa balozi mwema wa CRDB.

“Kwanza niwapongeze sana CRDB kwa sababu uamuzi wao ni sahihi, huyu jamaa anaweza kuwasaidia kuwafikishia ujumbe kwa mamilioni ya watu ndani na nje ya nchi.

“Mimi siyo shabiki wa Harmonize, lakini niliposikia tangazo alilowafanyia CRDB nilimpa alama mia,” alisema Bakari Shabani mkazi wa Masaki, Dar.

Naye Rafael Masunga wa Mbezi Beach, Dar aliipongeza Benki ya CRDB kwa kumpa shavu Harmonize akiamini kuwa mamilioni watakayomlipa yatamsaidia kupushi muziki wake.

Hivi karibuni CRDB waliingia mkataba na msanii huyo kwenye programu yao maalumu waliyoipa jina la Popote Inatiki.

Huduma hiyo ni maalumu kwa ajili ya kuhamasisha jamii kutumia zaidi huduma za benki hiyo kipindi hiki cha Corona kupitia mitandao na kuachana na utaratibu wa watu kupanga foleni kwenye matawi ya benki hiyo yaliyotapakaa nchi nzima, jambo ambalo limepongezwa na wengi.

STORI | Neema Adrian, Risasi Tazama

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post