TAARIFA mbalimbali katika vyombo vya habari nchini Uingereza leo zinasema kuwa mshambuliaji wa Taifa Stars na klabu ya Genk, Mbwana Samatta yukom mbioni kusajiliwa na klabu ya Aston Villa ambayo ipo katika nafasi ya 18 ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).
Kwa mujibu wa chanzo cha Daily Star na Mirror, Aston Villa inakaribia kumsajili Samatta kwa kiasi cha Pauni milioni 8.5, ambapo hii leo amefanya mazoezi na timu yake lakini anatarajiwa kusafiri hadi nchini Uingereza kukamilisha dili hilo.
Samatta (27) aliifunga bao moja Liverpool kwenye michuano ya Champions League na mpaka sasa amefunga mabao 76 katika mechi 191 alizoichezea Genk huku akiwa na mabao 20 katika mechi alizoichezea taifa Stars.
Samatta ambaye ambaye alikuwa akihusishwa kutua Crystal Palace yupo katika msimu wake wa nne katika klabu yake Genk, amekataa ofa mbalimbali kutoka klabu za Mashariki ya Kati akishinikiza uhamisho wa kwenda ligi kuu nchini Uingereza ambako ndio ndoto yake ilipo.
Bosi wa Aston Villa, Dean Smith amethibitisha kuwa klabu inahitaji kuongeza nguvu ya kikosi baada ya changamoto walizopata katika mzunguko wa kwanza, “tunalifanyia kazi hilo muda wote, ninafikiri tutakamilisha kabla ya Jumapili”, alisema wiki iliyopita.
Aston Villa iko katika nafasi ya 18 ya msimamo wa ligi kuu nchini Uingereza kwa sasa na inahitaji mshambuliaji wa kati baada ya kuumia kwa mshambuliaji wake, Wesley.
Tags
Michezo