Kutua kwa nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta katika kikosi cha Aston Villa, kunaambatana na neema nyingi, ikiwemo mshahara wake kupanda kwa zaidi ya mara tatu. Samatta alitambulishwa Aston Villa juzi Jumatatu na anakuwa mshambuliaji wa kwanza wa Afrika Mashariki kucheza kwenye Ligi Kuu ya England, ambayo ni kubwa na maarufu zaidi duniani.
Straika huyu ametua Villa akitokea KRC Genk ya Ubelgiji ambako alikuwa akilipwa mshahara wa euro 16,500 kwa wiki ambazo ni sawa na Sh milioni 42 za Kitanzania kila wiki. Sasa taarifa kutoka Aston Villa zinaeleza kuwa mshahara wa nahodha huyu wa Taifa Stars hautakuwa chini ya pauni 40,000 kwa wiki.
Championi linaendelea kuchimba na hivi karibuni litaibuka na data kamili. Kama akilipwa pauni 40,000 kwa wiki, hizi maana yake ni zaidi ya Sh milioni 119 za Kibongo ambazo atakuwa anakunja kila wiki na kuwa mmoja wa wachezaji matajiri zaidi Afrika.
Ni dhahiri kuwa kwa mshahara huo ambao si chini ya pauni 40,000 kwa wiki, Samatta anakuwa mmoja wa wachezaji wanaolipwa zaidi Aston Villa.
Mchezaji wa Aston Villa anayelipwa mshahara mkubwa zaidi, anapokea pauni 42,000 kwa wiki ambaye ni kipa Tom Heaton, akifuatiwa na kiungo Henri Lansbury (wote hawa ni Waingereza) anayepokea pauni 40,000 kila wiki, hawa ni wachezaji pekee wa Aston Villa waliofikisha mshahara wa pauni elfu 40 kwa wiki, wengine wako chini ya hapo. Maana yake Samatta atakuwa mmoja wa wachezaji wanaolipwa vizuri zaidi Aston Villa na huenda akaongoza kwa mshahara kama akipewa zaidi ya pauni 40,000 kwa kuwa mshahara wake kamili haujatajwa zaidi ya kuelezwa hautakuwa chini ya pauni elfu 40.
“Mshahara wake utawekwa wazi hivi karibuni lakini haitakuwa chini ya pauni 40,000 wala zaidi ya pauni 60,000,” kilisema chanzo cha ndani cha Aston Villa kilipozungumza na Championi Jumatano jana mchana. Mshahara huo wa Samatta unatosha kulipa wachezaji wote wa Simba kwa mwaka mzima kwa bajeti yao ya Sh bilioni 4 kama alivyoeleza Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, bilionea Mohamed Dewji.
Wachezaji wanaoongoza kwa mshahara Simba ni Meddie Kagere anayepokea Sh milioni 11 kwa mwezi, Clatous Chama (Sh milioni 8.7), John Bocco (Sh milioni 8), Gerson Graga (Sh milioni 8) na Aishi Manula (Sh milioni 7.5). hawa wote Samatta anaweza kumudu kuwalipa mshahara bila shida na akaendelea kuishi kifahari anavyotaka.
Kwa mshahara huo, pia Samatta ana uwezo wa kulipa mshahara wa wachezaji na wafanyakazi wote wa Yanga ambao bajeti yao ni Sh milioni 120 kwa mwezi. Anaweza kuwalipa kwa mshahara wake wa wiki tu na maisha yake mengine yakaendelea baada ya hapo.
Mshahara huo pia unamfanya Samatta awe na uwezo wa kununua fuso mbili ndogo kila wiki zenye thamani ya Sh milioni 60 kila moja Samatta ambaye atakuwa anavaa jezi namba 20, ameingia kwenye orodha ya wachezaji matajiri na wanaolipwa zaidi Afrika, na sasa fedha kwake siyo tatizo, labda tatizo liwe matumizi. Samatta ameondoka Genk akiwa ameifungia jumla ya mabao 43 katika mechi 98, anatarajiwa kufanya makubwa zaidi Aston Villa ambayo imemchukua aiokoe na janga la kushuka daraja.
Mechi yake ya kwanza kuonekana uwanjani, inatarajiwa kuwa ya nusu fainali ya pili ya Kombe la Carabao dhidi ya Leicester Jumanne ijayo Januari 28 lakini katika mechi ya Premier, Watanzania watamuona kwa mara ya kwanza Februari Mosi atakapovaana na Bournemouth ugenini. Watanzania watakuwa na nafasi ya kumshuhudia mtu wao akichuana na Liverpool, Arsenal, Chelsea, Manchester United na Tottenham katika mechi ya Premier msimu huu
Tags
MICHEZO KIMATAIFA