NI JAMBO jema sana kumshukuru Mungu. Mshukuru kwa uhai na afya aliyokupa kwani wapo wengi waliotamani kuwepo duniani lakini wameshakufa, wewe umempa nini Mungu? Ni kwa neema yake tu tunaishi.
Mwaka 2019 unaelekea ukingoni, bado siku chache mwaka uishe. Wapo ambao mwaka huu ulikuwa mzuri kwao kuanzia kwenye afya hata kimaendeleo.
Lakini wapo wengine ambao mwaka huu haukuwa mzuri kwao, ulikuwa wa majanga. Inawezekana ni kutokana na magonjwa, balaa na mambo mengine mbalimbali ambayo yalisababisha ukose amani na furaha katika maisha yako.
Kwenye makala haya leo tunakuletea mastaa ambao mwaka huu wamekutwa na majanga ya aina mbalimbali na kukosa furaha.
IDRIS SULTAN
Mchekeshaji huyu mwaka huu wa 2019 haukuwa mzuri kwake kwani alikutwa na majanga ya kuswekwa rumande katika Kituo Kikuu cha Polisi ‘Sentro’ baada ya kuweka picha yake ikiwa na sura ya Rais John Magufuli katika mtandao wa kijamii wa Instagram.
Idris alikaa rumande kwa saa kadhaa mpaka alipotoka kwa dhamana. Hivyo, akawa anaenda kuripoti polisi kila wiki.
MWEMBA BATONI ‘MWIJAKU’
Mwijaku ambaye ni msanii wa vichekesho, aliingia kwenye majanga baada ya kudaiwa kusambaza picha chafu za aliyewahi kuwa mpenzi wake, Menina Atick.
Msanii huyu aliswekwa rumande katika Kituo cha Polisi Oysterbay jijini Dar na baadaye kuachiwa kwa dhamana.
MENINA ATICK
Mwanamama huyu kutoka kiwanda cha muziki wa Bongo Fleva, alijikuta kwenye majanga baada ya video zake kusambaa mitandaoni jambo ambalo lilizua gumzo kila kona na kuwa aibu kwake.
Menina aliitwa Baraza la Sanaa la Taifa ‘Basata’ na kuhojiwa kisha kuendelea na kazi zake za kila siku japo mpaka leo hajulikani anajishughulisha na nini hasa maana kwenye muziki amepotea.
AUNT EZEKIEL
Katika kujikwamua kimaisha, msanii wa filamu Aunt Ezekiel alifungua pub ya kifahari na kutumia pesa kibao lakini kabla ya kufika mbali, alikutana na majanga ya kutakiwa kuifunga.
Aunt alipelekwa mahakamani kutokana na pub yake kudaiwa kuwapigia kelele wakazi wanaoizunguka. Hivyo kuifunga mpaka hivi karibuni alipoifungua tena.
IRENE UWOYA
Akiwa kwenye mkutano na waandishi wa habari, staa huyu wa filamu za Kibongo aliwarushia fedha ambapo kitendo hicho kilisababisha uharibifu wa baadhi ya vifaa vya kazi vya waandishi.
Kutokana na kitendo hicho, Basata walimwita Uwoya na kumuhoji ambapo alitakiwa kuwaomba radhi waandishi wa habari na akafanya hivyo.
SHAMSA FORD
Mwanamama huyu kutoka Bongo Muvi, anaingia kwenye orodha hii kutokana na majanga ya ndoa yake na Chid Mapenzi.
Shamsa aliachana na mumewe na sasa yupo singo akiendelea na maisha yake na hajaolewa tena.
FAUSTINA CHARLES ‘NANDY’
MSANII huyu wa muziki Bongo, alikutana na majanga mazito baada ya aliyekuwa mchumba wake, Ruge Mutahaba kufariki dunia.
Baada ya kifo cha mchumba wake huyo, Nandy aliweka wazi kuwa ilikuwa bado siku chache tu avalishwe rasmi pete ya uchumba lakini Mungu hakupenda.
MAKALA: Gladness Mallya
Tags
Udaku