BABA mzazi wa mshambuliaji wa KRC Genk ya nchini Ubelgiji, Mbwana Samatta, Mzee Ally Samatta, amemuandalia Jogoo mwanaye huyo pindi atakaporejea nchini hivi karibuni kutokana na furaha aliyokuwa nayo ya kuifunga Liverpool.
Samatta juzi aliitungua Liverpool katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo katika mchezo huo Genk ilipokea kichapo cha mabao 2-1.
Kwa sasa Genk inashika mkia katika kundi lao E ikiwa na pointi moja na Liverpool ikiongoza ikiwa na pointi tisa. Akizungumza na Spoti Xtra, Mzee Samatta amesema kuwa; “Nililala nikiwa nimenenepa sana
kwani nilifurahi sana kuona bao lake limerudi, lile la awali walimnyima na VAR lakini Mungu ameonyesha miujiza amemrejeshea bao lake tena kwa staili ileile ya kichwa.
“Furaha yangu leo (jana) nakula ugali wa muhogo na jogoo mkubwa, najisikia furaha sana na naendelea kumuombea kwa Mungu.
“Nasubiria akirudi nyumbani kati ya tarehe 9 au 10 niweze kumchinjia jogoo mkubwa ambapo ni sehemu ya zawadi kwangu na kumpongeza kwa kazi anayoifanya, kwa jinsi hali ilivyo angepata wasaidizi wazuri kama walivyo wa Liverpool angeweza kufunga mabao mengi lakini tatizo wasaidizi aliokuwa nao hawapo vizuri sana japo wanasaidiana vyema,” alisema Mzee.
Tags
MICHEZO KIMATAIFA