WAKATI joto lilikuwa likifukuta Simba kati ya mwekezaji wa klabu hiyo Mohammed ‘Mo’ Dewji’ dhidi ya Mwenyekiti Swedy Mkwabi, jana serikali imetoa tamko juu ya uwekezaji ndani ya klabu zote ikiwamo Simba, ikiwa kama mtego wa bilionea huyo.
Jana Jumatano serikali imetoa muongozo wa mfumo wa uendeshaji wa klabu za soka nchini zilizoanzishwa na wananchi kwa kubainisha asilimia 49 ya hisa anazopewa mwekezaji hazipaswi kuhodhiwa na mtu mmoja.
Tayari Simba ilishamtangaza Mo Dewji kuwa mwekezaji mwenye hisa hizo 49 kwa thamani ya Sh20 bilioni, huku Yanga ikiwa njiani nayo kuingizwa kwenye mfumo wa kampuni, lakini mchakato wao ukiwa bado haujawekwa bayana licha ya katiba kuutambua mfumo mpya.
Hata hivyo, jana, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe katika mkutano wake na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) alisema asilimia 49 ya hisa hazipaswi kuhodhiwa na mwekezaji mmoja.
Waziri Mwakyembe alisema katika uwekezaji huo tatizo limejitokeza katika mgawanyo wa asilimia 49 ya hisa kanuni za Baraza la Michezo la Taifa (BMT) zinataka hisa hizo zisihodhiwe na mtu mmoja bali wawekezaji wawe watatu au zaidi. “Kazi ya kuweka utaratibu gani wa hizo asilimia 49 tuliiachia TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) ifanye kwa mujibu wa kanuni, lakini hiyo kazi haikufanyika mpaka sasa (jana mchana),” alisema Dk Mwakyembe.
“Nimeshauri iundwe kamati ndogo ya wataalamu ili kuweka kanuni vizuri ambapo katika kamati hiyo kutakuwa na mjumbe mmoja kutoka BMT, TFF, Kurugenzi ya Michezo, mwakilishi wa wadau, TRA (Mamlaka ya mapato Tanzania) na wajumbe wawili kutoka Soko la Hisa na Mitaji,” alisema.
Akizungumzia tamko la Dk Mwakyembe, aliyekuwa Kaimu Rais wa Simba aliyeongoza mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema hajalisikia na kama lipo “wacha lije hakuna shida.”
Naye mwanasheria, Alex Mgongolwa alisema kama agizo limetolewa na Serikali, klabu zinazoelekea kwenye mfumo huo hazina budi kufuata.
Leo Alhamisi, aliyekuwa mwenyekiti wa Baraza la Wadahamini la Simba, Hamis Kilomoni amepanga kuzungumza na wanahabari nyumbani kwake kuzungumzia jambo hilo, ikiwa ni siku chache tangu Wakala wa Usajili wa Ufilisi na Udhamini Tanzania (Rita) watangaze kutomtambua tangu mwaka 2017.