Wachezaji hao wawili wamekosa vipindi viwili vya mazoezi juzi na jana usiku baada ya kuumia katika mchezo dhidi ya Kenya.
Cairo, Misri. Pigo kwa Taifa Stars baada ya kuthibitika kuwa beki Kelvin Yondani na kipa Aishi Manula wataukosa mchezo wa leo kati ya Tanzania dhidi ya Algeria kwenye Uwanja wa Al- Salam nchini Misri.
Mchezo huo wa mwisho wa Kundi C, hauna maana yoyote kwa Tanzania zaidi ya kusaka kuweka rekodi kwa kuwa wameshatolewa huku Algeria ikiwa imefuzu kama kinara wa kundi hilo
Wachezaji hao wawili wamekosa vipindi viwili vya mazoezi juzi na jana usiku baada ya kuumia katika mchezo dhidi ya Kenya.
Daktari wa Taifa Stars, Richard Yomba amesema Yondani na Manula afya zao zimeshindwa kuimarika mapema kabla ya mchezo wa leo usiku.
Yomba alisema wawili hao baada ya kupata maumivu katika mchezo dhidi ya Kenya kitengo chake kilipambana kuhakikisha wanakuwa tayari, lakini imeshindikana.
Alisema wamelazimika kuwaondoa katika kikosi kitakachocheza mechi ya leo kwa kuwa bado wanaendelea na matibabu zaidi.
Aidha Yomba alisema ukiondoa Yondani na Manula wachezaji wengine wote wako sawa kuelekea mechi hiyo.
Mapema Kocha wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike alisema bado ana matumaini timu yake ina nafasi ya kufanya vizuri katika mchezo huo.
Amunike alisema licha ya Algeria kuwa na kikosi kizuri, lakini bado ana matumaini makubwa na vijana wake kuwa watafanya vizuri katika mchezo huo wa mwisho wa kundi C.
“Tumecheza na Algeria mara kadhaa, nakumbuka mchezo wa Dar es Salaam tuliocheza tukafungwa 2-0, na baadaye tukaja kucheza nao tukatoka sare 2-2, nakumbuka pia walikuja wakatufunga mabao 7-0, lakini hiyo yote ni historia,”alisema na kuongeza:
“Kwasasa hivi tunachokitazama ni namna gani tutaweza kusawazisha makosa yetu yaliyotokea katika michezo miwili iliyopita, na kufanya uamuzi sahihi tunapokuwa na mpira, kwahiyo Jumatatu ni ukurasa mwingine na ni safari nyingine kwa Tanzania na Algeria, na hauwezi kutabiri nani atakuwa mshindi, kwahiyo tutaingia uwanjani kupambana na kusaka pointi tatu,” alisema Amunike.
Taifa Stars itaivaa Algeria ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa na Senegal mabao 2-0 pamoja na Kenya mabao 3-2.