ILE mipango ya Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera ya kuanza usajili mapema, sasa imesimama mpaka hapo baadaye.
Hivi karibuni, ilidaiwa kuwa Zahera alitarajiwa kupewa fedha za kuanza usajili kutoka kwa kamati ya klabu hiyo inayosimamia zoezi la ukusanyaji fedha kutoka kwa wanachama wa klabu hiyo kwa ajili ya usajili wa wachezaji watakaoitumikia timu hiyo msimu ujao.
Kamati hiyo ambayo inaongozwa na Mbunge wa Dodoma Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kazi, Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Walemavu, Antony Mavunde, inaelezwa kuwa ilipanga kumpatia Zahera kiasi cha Sh milioni 300 kwa ajili ya usajili.
Hata hivyo, habari za ndani ya Yanga ambazo Championi Jumamosi limezipata, zimedai kuwa mpango huo umesimamishwa kwa muda mpaka hapo uchaguzi mkuu wa klabu hiyo utakapomalizika.
Uchaguzi huo wa viongozi wapya wa klabu hiyo, umepangwa kufanyika Mei 5, mwaka huu.
“Zoezi la usajili ambalo kocha alikuwa anatarajia kuanza hivi karibuni limesimama kwa muda, ila ameambiwa kama kuna wachezaji anawataka basi aendelee kufanya nao mazungumzo.
“Fedha za usajili alizoomba atapewa baada ya kumalizika kwa uchaguzi kwani hivi sasa inakuwa ni ngumu kuanza kufanya usajili bila ya kuwepo kwa uongozi ambao ndiyo utakuwa ukisimamia mambo yote ya fedha,” kilisema chanzo. Hata hivyo, Zahera alipoulizwa kuhusiana na suala hilo, aligoma kulizungumzia.
Lakini alipotafutwa katibu mkuu wa kamati hiyo ya kuichangia Yanga, Deo Mutta ili awaze kulizungumzia hilo alisema: “Nipo kwenye kikao kwa hiyo siwezi kuongea chochote kwa sasa.”
Hata hivyo, wakala wa mshambuliaji wa Gor Mahia ya Kenya, Jacques Tuyisenge ambaye Yanga wanadaiwa kumwania, Patrick Gakumba alipoulizwa kama tayari wameshamalizana na Yanga alisema: “Kuna mabadiliko kutoka Yanga, tulipanga kukutana hivi karibuni kwa ajili ya Tuyisenge lakini wameniambia nisubiri mpaka uchaguzi utakapomalizika ndipo watakapokuja Rwanda tumalize biashara.”