Shirikisho la soka nchini Tanzania TFF limeipiga faini ya 500,000 (laki tano) klabu ya Yanga kutokana na vurugu ilizowafanyia waamuzi wa mchezo wa Ligi Kuu kati ya timu hiyo na Ndanda FC.
Vurugu hizo zilitokea katika mchezo wa Ligi Kuu kati ya timu hiyo na Ndanda FC mjini Mtwara, na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Adhabu nyingine, Yanga imetozwa faini ya sh. 3,000,000 (milioni tatu) kutokana na timu yake kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi katika mechi hiyo iliyofanyika Aprili 4, 2019, huku Ndanda FC ikitozwa faini ya 1500,000 (milioni moja na laki tano) kwa kosa hilohilo.
Hilo ni kosa la nne msimu huu kwa timu ya Yanga kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi, na adhabu dhidi yake imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Taratibu za Mchezo.
Wakati huo huo, mlinzi wa Yanga, Kelvin Yondani amefungiwa mechi tatu na kutozwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumpiga ngumi mchezaji wa Kagera Sugar FC katika mechi iliyochezwa Aprili 11, 2019 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, huku Aggrey Morris wa Azam FC amefungiwa mechi tatu na kutozwa faini ya 500,000 baada ya kutolewa nje kwa kumpiga mchezaji wa Mbeya City.
Adhabu hiyo ni kwa kuzingatia Kanuni ya 38(9) ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.