***KIMINI CHA MTOTO WA ASKOFU***
Sehemu ya 2;
Kwa wasomaji wapya, ‘KIMINI CHA MTOTO WA ASKOFU’ ni simulizi halisi ya mambo yaliyotokea katika maisha inayokusanya matukio halisi ama yanayosimamia ama kujengwa katika uhalisia. Juma lililopita nilielezea jinsi nikitoka uwanja wa ndege gari letu lilivyogonga gari la binti mmoja aliyekuwa amevaa kimini. Binti huyo baada ya kuona gari lake limekwanguliwa alimtukana sana dereva aliyekuwa ananiendesha. Katika purukushani hilo, akatokea mtumishi wa Mungu kumbe anamfahamu yule binti. Naye binti baada ya kumwona alibadilika ghafla na kujifanya mwema kisha wakasalimiana na yule mtumishi ‘Bwana Yesu asifiwe’, wakachangamkiana na maelewano yakatokea kila mmoja akaenda safari yake. Nami nikapelekwa hotelini. Baada ya kupewa chumba, nilipokuwa napanda ngazi macho yangu yakagonga na binti ambaye alikuwa si mgeni kwangu. Nikaweka mizigo yangu chumbani nikaamua kushuka pale mapokezi. Sasa endelea…,.
Basi wakati nilivyokuwa nashuka nikamkuta tena yule binti pale mapokezi akidai mzigo wake, sasa ikanibidi nipitilize kwanza kwenda wanakouza chakula, kisha nimalizie hapo...basi ninaporudi akawa ameshaondoka. Sasa nikiwa pale mapokezi nikamsikia yule kijana wa mapokezi akisema "Mabinti wengine jamani! Sijui wanakosa nini aisee?" basi nikadakia "Kwanini kaka?"
Basi akashusha pumzi na kusema "Kaka wewe acha tu,mambo mengine ni magumu sana kuamini ila hapa wanakuja Watumishi mbalimbali, wahubiri na hata waimbaji kadhaa wa injili na watu wengine maarufu, hapa ndio kijiwe chao....na hata huyu binti aliyetoka hapa, Nasikia ni Mtoto wa mheshimiwa mmoja serikalini, tena ni mtu mashuhuri sana na huyu binti huwa anakuja mara nyingi tu hapa wazee mbalimbali! “Mmh sasa amekosa nini kwao binti huyu?” Niliuliza! Kwa kweli ni vigumu kujibu hilo lakini unajua kaka, watoto wengi ambao kwao wana kila kitu wengi hawajatulia.
Nadhani walikuwa wanafungiwa geti kali sana wakati wanakua hivyo wanataka kuwaonyesha wazazi wao kuwa wana uhuru na maisha yao au ni kufuata mkumbo au ujinga tu maana hata mimi sioni sababu! Alijibu yule kaka wa mapokezi kwa urefu.
“Mimi nafikiri haya ni mapepo tu wala hakuna kingine, amefungwa ufahamu wake, anaendeshwa moyo wake na mwili wake unatumikishwa,” basi akaniangalia na kusema, labda kweli, maana kwao nasikia wana kila kitu ambacho mtu angetamani kuwa nacho!, Lakini hapa duniani kuna mengi huwezi kujua, kama je alipatikana kwa dawa ama labda utajiri na umaarufu wa baba yake ndio unaugharimu usichana wake je? Aliuliza yule mhudumu! Oooh kumbe! Nikatamani kuuliza jina la yule binti ila nikajiambia moyoni, haina haja sana, basi nikapatiwa vile nilivyoviomba na kisha nikapanda zangu juu chumbani kwangu kwenda kula na kulala!
Nilipofika chumbani kwangu baada ya kula niliamua kupumzika kidogo, baadae kidogo niliamua kwenda bafuni kuondoa uchovu, nikaoga na kukaa ili angalau nijiburudishe, nikawasha televisheni ili kujaribu kuangalia ulimwenguni kunaendelea nini. Nilipowasha kwenye umeme, televisheni haikuwaka, nadhani ni kwa sababu ilizimwa kwa rimoti, hivyo ikanibidi nitafute rimoti, nilitupia macho huku na kule sikuiona mezani wala kwingine haraka, ikanibidi nianze kutafuta huku na kule, nilipofungua droo zote za kitanda na makabati sikuipata ila nikakuta lundo la mipira ya kiume ya kila aina, Kha! Nikashtuka kiasi, lakini nikajiambia moyoni labda ndio sera za nyumba za wageni za mjini, kuwalinda wateja wao dhidi ya maambukizi, lakini pia nikahisi kuna mtu ama watu huwa wanapendelea sana chumba kile na kwa kuwa wanakuja mara nyingi, basi hujiwekea akiba. Kwenye droo nyingine nikakuta jarida la picha za wanawake wa kizungu wako uchi kabisa. Bila shaka jarida lile lilikuwa linahusiana na mitandao ya biashara za ngono za huko ughaibuni, Tanzania haliwezi kuuzwa kwa sababu ya sheria, hivyo aliyelileta ama kulisahau, lazima amelitoa mbali huko kwa njia magendo! Mmmh! Nikasikia hasira ndani yangu! Nikajiuliza maswali mengi bila majibu hivi leo ndio nimeibukia wapi huku!
Nilichoka nikaa kitako na kuanza kujikuta nikiomba rehema maana nimeingia mahali ambapo sikukusudia kabisa, Nilimsihi sana Mungu akili yangu isivurugike na mapepo na maagano yote katika chumba na nyumba ile yasiambatane nami kamwe. Ni muhimu kujitenga na madhabahu na maagano ya kishetani mahali popote unapokuwepo, maana huwezi kujua kabla ya wewe ni nani alikuwepo na alikusudia nini na alifanya agano maagano gani yanayoweza kukugusa na wewe kama usipokuwa na ulinzi mwingine….Nikayakumbuka maneno ya mtumishi mmoja niliyewahi kumsikia!
Nilijitahidi kubaki mstarini bila kupoteza dira na kwa hakika niliweza, ukizingatia kesho yake nilikuwa nina harusi ya mpendwa mmoja hivi wa kule kanisani, hivyo niliendelea na maombi na maandalizi ya rohoni kwa habari ya kazi nilizokuwa nazo mbeleni na kwa upande wangu. U-mc ni Utumishi kabisa, nimekuwa naamini katika furaha, mafanikio na kibali cha Mungu katika shughuli yeyote ninayokuwepo. Jumamosi nilikuwa nina harusi na Jumapili nilikuwa ninaongoza Ibaada ya kuwekwa wakfu kwa mkanda wa video wa mwimbaji fulani maarufu wa injili katika kanisa fulani la Pentekoste hapa mjini...Sasa nikaona haya matakataka nionayo yanayotaka kunikumbusha enzi zile za kale, kabla sijamgeukia Mungu na kuwa mtumishi. Sasa ndio nini? lakini nikajiambia moyoni, neema ya Mungu inatosha, ngoja niwe mtulivu yamkini kuna jambo la kujifunza hapa maana kuna jambo la kujifunza kwenye kila litokealo maishani mwetu kama tukiamua kujifunza!
Nilihisi mazingira haya sio rafiki sana na hivyo kabla sijavurugikiwa zaidi, ikanibidi nitoe kompyuta mpakato (Laptop) yangu niweke mezani, angalau humu nitasikiliza nyimbo za kuabudu na kujenga mazingira ya Ibaada nikiwa humu hotelini. Basi nikaiwasha na kuweka nyimbo hapo, maana nilikuwa na nyimbo zaidi ya elfu moja. Zikiwa zinaendelea nikajikuta naaanza kutafakari maneno ya yule mhudumu na yule binti aliyenisalimia kikristo wakati nafika. Mhudumu alisema hapa wanakuja watumishi wengi tu! Sasa wanakuja kufanya nini hapa kama ndio kumekaa kidhambidhambi namna hii? Nikawa na maswali mengi kichwani, inawezekanaje watumishi wapende mahali hapa penye uchafu namna hii?
Basi nikiwa natafakari bila kupata majibu, na mara usingizi ukanichukua!
Nikiwa ndani ya lindi la usingizi niliota ndoto, siikumbuki yote kwa usahihi ila angalau yako mambo ninayakumbuka katika mojawapo ya ndoto zile hata leo;
Ndoto yenyewe ilikuwa hivi:
NILIKUWA NATEMBEA MAHALI FULANI NA NIKAONA JENGO MOJA KAMA UKUMBI ILA WATU WALIO MAENEO HAYO NI KAMA WATUMISHI HIVI NA KAMA VILE KULIKUWA NA SEMINA, BASI NA MIMI NIKASEMA NGOJA NIULIZIE HAPA KUNA NINI,YAMKINI NIKAPATA UKUMBI WA KUFANYIA MATAMASHA YANGU,
NILIPOSEGEA KARIBU NIKAONA KAMA NI NYUMBA YENYE VYUMBA VINGI SANA NA INA KORIDO MOJA NDEFU YENYE GIZA GIZA....NIKIWA NATEMBEA KUUKARIBIA MLANGO WA KWANZA NIKIAMINI LABDA NDIO MAPOKEZI, NIKASIKIA KAMA SAUTI YA MAOMBI,KAMA VILE WATU WANANENA,NILIPOFUNGUA MLANGO NIKAONA
MWANAUME MMOJA YUKO NA WANAWAKE KAMA SITA HIVI WAKIWA WATUPU NA WANAFANYA MAPENZI NA YULE MWANAUME NI KAMA NINAMFAHAMU,BASI NIKAFUNGA KWA KUSHTUKA SANA....MMMH! NIKAJIAMBIA YAMKINI NIMEKOSEA MLANGO,BASI NIKAPIGA HATUA ZAIDI KUUKARIBIA MLANGO WA PILI, HUMO NIKASIKIA SAUTI YA MAHUBIRI TOKA KWENYE RADIO AU
TELEVISHENI,NILIPOFUNGUA MLANGO NIKAWAONA WATUMISHI KADHAA WAMEKAA WANAANGALIA NGONO...YAANI SAUTI NI MAHUBIRI ILA PICHA NI NGONO, BASI NIKAWAULIZA SASA HUO NDIO UPUUZI GANI MNAOFANYA? MMOJA AKANIJIBU USIJALI MTUMISHI,TUKO HAPA TUNAANGALIA JINSI GANI SHETANI ANAVYOUHARIBU ULIMWENGU, MMH NIKAUFUNGA ULE MLANGO NIKAKIMBIA
KWENYE ILE KORIDO ILI NIPATE CHUMBA NIPUMZIKE...NIKAONA MLANGO MBELE YANGU NIKAUFUNGUA NA NIKASIKIA SHINDWA KWA JINA LA YESU,NIKAUFUNGA, NILIPOCHUNGULIA NI KAMA VILE WAKRISTO WAMEJITENGA HUMO KWA UOGA NA HAWATAKI KABISA KUSIKIA CHOCHOTE,HIVYO KILA KINACHOINGIA WAO
WANAKEMEA KABISA...BASI NIKAFUNGUA MLANGO MWINGINE NA HAPO NIKAONA KAMA MADHABAHU ILA IMEJAA VUMBI MNO,NA NILIPOANGALIA VIZURI,NIKAONA KAMA KANISA LA MIAKA MINGI SANA AMBALO LIMETELEKEZWA, NIKAONA KITI,NIKAKIFUTA ILI NIKAE,NACHO KIKAVUNJIKA MAANA KIMEOZA, BASI
AKAINGIA MTU MMOJA MSAFI SANA ILA NI KAMA HAJAPIGA MSWAKI,NAYE AKANIAMBIA...WENZAKO HUMU HUWA HAWAKAI,TAFUTA VYUMBA VIZURI HUKO NJE UKAKAE NA WATUMISHI WENZAKO! NDANI YANGU NIKAJISIKIA HASIRA NA NIKAMWAMBIA..WEWE NI NANI HATA UNIHOFIE MIMI KUKAA HUMU? AKACHEKA! BASI NAMIMI NIKAMWAMBIA YESU NINI YOTE HAYA NIONAYO? NIKASHANGAA AMEBADILIKA SURA MTU YULE NA KUTOKA HARAKA, WAKATI ANATOKA
ALIBAMIZA MLANGO KWA NGUVU
na hapo nikashtuka kumbe na Dirisha sikufunga na lenyewe ndio lilijibamiza kwa nguvu kwa upepo pia!
Basi niliposhtuka nikaangalia saa, ilikiwa saa tisa na dakika arobaini...nikawaza hivi hii ndoto maana yake nini? Dirisha likaendelea kujibamiza ndio hapo nikasogea ili nifunge dirisha na hapo nikaiona rimoti dirishani, kwamba imefikaje dirishani hata mimi sijui ila nikaichukua na kufunga dirisha...na kisha nikajaribu kuwasha televisheni, anagalau nijue nini kinaendelea huko.
Chaneli ya kwanza nikaona Mpira, ya pili nikaona muziki, ya tatu nikaona mieleka, basi nikaendelea ya nne nikaona kama filamu, ya tano nikaona ngono, ya sita ngono, ya saba ngono, ya nane muziki, ya tisa wanyama na ya kumi chenga, nikaendelea mbele nikaona zinajirudia duh! Basi nikazima maana nilitamani nione angalau BBC au Aljazera au kingine chochote ila sio hayo matakataka!
Jamani! Sasa hao watumishi, hao waimbaji, na yule niliyepishana naye na yule binti pia humu ndani wamevutwa na kitu gani hasa?
Nikarudi kwa kompyuta mpakato yangu tena maana huku tu ndio kumebaki salama, Na kwakuwa ilikuwa imewashwa muda mrefu, chaji ilikuwa imekwisha kabisa, hivyo nikatoa chaja kwenye begi na kutafuta mahali pa kuchomeka ili angalau nifanye maandalizi ya ratiba ya kesho yake.
Soketi ama Sehemu za kuchomeka zote zilizokuwa zinaonekana, za Umeme zilikuwa zimejaa, hivyo ikanibidi niangalie kama ipo nyingine upande mwingine na hapo nikaiona kwa mbali ukutani, mahali ilipokuwepo nisingeweza kuchomeka mapaka kwanza kitanda kisogee kidogo na hiyo ikanibidi nivute kitanda ili niweze kuchomeka chaja ya kompyuta ile, Nilipovuta tu Kitanda mara nikasikia kitu kimeanguka chini, Nikasogea, nikainama na kukiokota kitu hicho!
Khaaa! Kumbe ni pochi ya kiume, nikaikota na kuifungua ili nijue ni ya nani hasa!
Yaani sikuamini nilichokiona Duh! Nilipoifungua tu nikaka kitandani n ahata kusahau nilichokuwa ninakifanya kabla ya kuiona pochi ile.
Kwa ushahidi wa vitambulisho, kadi mbili za benki, hela laki moja na ishirini na tatu, pesa tasilimu, kadi za mawasiliano za watu mashuhuri, yaani kusema ukweli niliishiwa pozi, Sitaki kuamini kama ile pochi ilikuwa ya..........ITAENDELEA
Tags
SIMULIZI