KOCHA wa Yanga Mwinyi Zahera amesema kuwa yeye ndiye alimtimua meneja wa timu hiyo, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ baada ya kuonekana kwenye ofisi ya Mwekezaji wa Simba, Mohamed Dewji Mo licha ya yeye kufafanua kuwa alikuwa na ishu zake.
Lakini siyo hilo tu, Zahera amemhusisha staa huyo wa Zanzibar mwenye heshima Yanga na bao walilofungwa na Meddie Kagere kwenye mechi ya mwisho ya watani.
Cannavaro ambaye baada ya kustaafu soka mwishoni mwa msimu uliopita alikabidhiwa cheo hicho, ametimuliwa na kocha huyo kwa madai kuwa anawasaliti na amekuwa na washikaji wengi sana wa Simba katika miezi ya hivi karibuni.
Zahera ameliambia Championi Jumatano kuwa, amefikia uamuzi wa kumtimua baada ya kufuatilia matendo yake kwa muda mrefu, lakini kubwa ni hilo la kuonekana kwenye ofisi ya bosi huyo wa Simba wakati Yanga ikiwa kwenye mapambano.
Mbali na sababu hiyo, pia Zahera anadai Cannavaro aliihujumu Yanga kabla ya kucheza na Simba Februari, mwaka huu na kufungwa bao 1-0 ambapo akiwa kama meneja, aliwaruhusu wachezaji kutoka usiku bila ya kocha kufahamu kitu chochote.
“Cannavaro hayupo kwa sababu alionekana katika ofisi ya bosi wa Simba anaingizwa mlango wa nyuma, watu walimuona, wakapigiwa simu viongozi wa Yanga kuambiwa kuwa Cannavaro, ameonekana akiingia katika ofisi ya bosi wa Simba, jioni alipoulizwa alisema kuwa alienda kumtafutia mke wake kazi.
“Lakini hili ni tukio la mara ya pili tulikua Morogoro kujiandaa na mechi ya Simba na siku mbili kabla ya mechi aliwaruhusu wachezaji watatu saa mbili na nusu usiku kwenda kukimbia mbio nje ya hoteli, waende hadi mjini bila ruhusa yangu.
Zahera aliongeza kuwa: “Kesho yake yule mtu wa ulinzi akaniambia kwamba Cannavaro aliruhusu wachezaji watatu kutoka usiku waenda kukimbia mbio, nikamuuliza walitoka dakika ngapi, mlinzi alisema hawakuchukua hata dakika 15 wakarudi.”
“Sasa siunaona kuna tatizo hapo nadhani siwezi kukubali mtu kama huyo katika benchi langu kutokana na mambo hayo,” alisema Zahera.
Hata hivyo, alipotafutwa Cannavaro simu yake haikupatikana huku ikidaiwa kuwa amekuwa akitumia simu ya ndugu yake kwa ajili ya kuwasiliana na watu wake wa karibu na hakuna ambaye tupo tayari kutoa namba hiyo.
Cannavaro ni mmoja kati ya wachezaji wa zamani wa Yanga ambapo alicheza kwa zaidi ya miaka kumi akiwa ametwaa makombe kadhaa makubwa.
CHANZO: CHAMPIONI