MAMBO 5 YA KUZINGATIA SIKU YA KWANZA KUONANA NA MPENZI WAKO


NI dhahiri kwamba mapenzi ni maisha na vita yake haijawahi kumuacha mtu salama, uwemwanajeshi, mbunge, kinyozi, au hata komando bado tu utaingia katika ulimwengu wa huba.

Unaweza kukutana na mpenzi mahali popote pale, iwe kwenye nyumba za ibada, sokoni,barabarani, kwenye magari, makazini, vyuoni na kama mtalisimamia vyema penzi lenu basi ni rahisi kuifikia hatua ya ndoa.

Baada ya siku ile ya kwanza mliyokutana ambayo haikuwa rasmi, mkabadilishana mawasiliano na mkaanza kuchati na kupigiana simu huku mkipanga mipango ya kukutana rasmi kwa ajili ya maongezi na kujuana zaidi. Yapo mambo mengi ya kuzingatia siku ile rasmi ya kukutana ambayo usipokuwa makini nayo ni rahisi kumpoteza huyo mwenzi wako ambaye huenda alikuwa na malengo mazuri kwako.

Muonekano: katika kipindi cha kuchati unaweza kugundua baadhi ya vitu ambavyo mwenzako anavipenda na asivyovipenda, ikiwemo ni aina gani ya mavazi anapenda uvae na uwe na muonekano upi. Kama ukifanikiwa kujua nenda na muonekano ule anaoupenda ilimradi tu uwe wa heshima. Ukishindwa kugundua basi nenda na muonekano mzuri ukiwa umependeza lakini usishushe heshima yako. Kwa upande wa wanawake, epuka kupaka ‘make-up’ hadi ukatisha, zingatia tofauti kati ya muonekano wa usiku na mchana, usivae kama dansa wa Fally Ipupa.

Kuongea sana: Jambo la pili muhimu la kuzingatia ni kuepuka kuongea sana mara baada ya kuwasili eneo husika mlilokubaliana kukutana. Hii ni kwa sababu ndiyo siku ya kwanza mnakutana, hakuna haja ya kuongea sana kujielezea kila kitu kuhusu maisha yako. Kwani ndani ya nusu saa mtu anakuwa ameshajua kila kitu kuhusu wewe. Wanaume hupendezwa sana na wanawake wapole na wasioongea sana kama chiriku. Kwa nini humpi mwenzako nafasi, muda wote unaongea wewe? Unataka kujua kila kitu kuhusu yeye kwa siku moja, msomaji wangu usitegemee kama ukitoka hapo huyo mtu atakutafuta tena.

Historia za wapenzi wenu wa zamani: Hapohapo kwenye maongezi si vyema sana kuelezana historia za maisha yenu ya kimapenzi yaliyopita kwa siku ile ya kwanza, kwa mfano, unamuelezea mwenzio kwamba ulishakuwa kwenye mahusiano na wapenzi watano tofauti na wote wakafariki. Unategemea akitoka hapo anaondoka na picha gani akilini mwake? Lazima utampa woga na atafikiria kwamba endapo ataendeleza mahusiano na wewe basi atakuwa wa sita kufariki. Moja kwa moja unamkimbiza ndege wako. Kikubwa cha kuongelea ni kuhusu nyinyi na kwa jinsi gani mnaweza kustawisha penzi lenu changa.

Tamaa: Miongoni mwa sababu inayoweza kuvunja mahusiano ni tamaa, si dhambi kutamani, lakini ni lazima ifahamike kwamba tamaa yoyote ile ikizidi ina madhara. Yaani ndiyo umefika tu umepewa nafasi ya kuagiza, ulivyo na tamaa unaagiza vitu vingi na vingine vya kubeba upeleke nyumbani. Kitendo cha kukuta mwenzi wako kapaki gari ya bei mbaya aina ya Range Rover unajua tu ana pesa, basi unaanza kumuorodheshea mambo kibao akufanyie. Kila biashara unataka akufungulie, kakukuta na simu ya tochi kisa umemkuta na iPhone mbili basi unaomba moja, yaani ni fujo tu. Baada ya hapo huyo mwanamme utamsikia kwenye redio; harudi ng’o!.

Ngono: Kuna madhara makubwa ya kufanya mapenzi siku ile ya kwanza ya kuonana. Ukiachilia mbali uwezekano wa kuambukizwa magonjwa ya zinaa likiwemo gonjwa hatari la Ukimwi. Hii ni kwa sababu ndiyo siku ya kwanza mmepata nafasi nzuri ya kuonana na siyo kweli kwamba mtaanzia hospitali ili kucheki afya zenu. Lakini pia mimba zisizotarajiwa , halafu mwanamme akakukimbia kwani humjui vizuri , hupajui kwa ndugu zake wala marafiki zake. Isitoshe atakuwa hapatikani kwenye simu, matokeo yake unabaki kulea mimba isiyo na baba ,

Ni vyema kuvutiana subira mjuane vizuri , mjihakikishie usalama wa afya zenu na mkiweza msubiri hadi mfunge ndoa kama Mwenyezi Mungu alivyoagiza kwani kuzini ni dhambi,

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post