Unamkumbuka Mchezaji Mtanzania Adam Nditi wa Chelsea...Alipo sasa


Bila shaka unalikumbuka jina la beki wa kushoto wa zamani wa Timu ya Vijana ya Chelsea U-21, Adam Nditi mwenye asili ya Tanzania. Hakuna aliyedhani angeweza kupotea kwenye ramani ya soka tena kirahisi kabisa. 

Nditi alizaliwa kwenye familia ya soka kutokana na baba yake Mzee Erick Nditi kucheza soka kipindi chake akiwa na Kikwajuni pamoja na Timu ya Taifa ya Zanzibar. 

Mzee huyo aliondoka Tanzania mwaka 1995 na kuzamia England baada ya kukutana na mrembo Marina, ambaye ana asili ya Italia na England. Alifikia katika Kitongoji cha Basingstoke. Wakati huo tayari alikuwa ameshaacha mtoto mmoja Zanzibar, ambaye ni Adam aliyezaa na mwanamke mmoja wa Kitanzania mwaka 1994 wakati akikaribia kuacha soka pale Kikwajuni. 

Kutokana na mzee wake kuwa Uingereza kulikuwa na wepesi kwa Adam naye kutua nchini humo na mara, baada ya kutua alikuwa akijihusisha na soka na baadaye akapata nafasi ya kujiunga na akademi ya Chelsea. 

Alijiunga na akademi hiyo mwaka 2016 kwenye kikosi cha vijana U-18 ambacho kilikuwa na vijana wenzake kama vile Charly Musonda Jr, Andreas Christensen na Ruben Loftus-Cheek. 

Umri ulivyosogea alipandishwa hadi kikosi cha U-21 cha Chelsea ambacho huwa kinashiriki Ligi Kuu England kwa vijana wenye chini ya umri huo. 

Akiwa na kikosi hicho cha Chelsea alipata nafasi ya kucheza mara kwa mara na moja ya michezo ambayo alicheza ni ule wa nusu fainali ya Kombe la FA, Aprili 10, 2011 kati ya timu yake iliyokuwa ikichuana na Manchester United. 

Kikosi cha United hiyo kilikuwa na Paul Pogba, ambaye kwa sasa anatesa kwenye kikosi hicho kinachonolewa na Jose Mourinho. 

Maisha yaliendelea kwa Adam na mwi showe akaingia katika kikosi cha kwanza cha Chelsea akipewa jezi namba 47, lakini kwa bahati mbaya ndipo ulipokuwa mwanzo wake wa kupotea. 

Adam alijikuta akitemwa mara baada ya kutoonyesha kiwango kizuri kwenye mazoezi ya kikosi hicho cha matajiri wa London na alipoondoka Chelsea alikaa kwa kipindi kirefu bila ya kupata timu ndipo alipoibukia Fleetwood, iliyokuwa daraja la pili (League One). 

Aliichezea kwa kipindi kifupi na mara baada ya mkataba wake kumalizika alitemwa na akajiunga na Farnborough ambayo aliichezea kwa miezi minne. 

Msimu wa 2016/17, Adam alijiunga na Guildford City na baadaye akapotea kabisa kwa kuishia mchangani. Huyu ndiye Adam, ambaye alikuwa anapigiwa chapuo la kuichezea Taifa Stars. 

Lakini, kwa bahati mbaya kupotea kwake pindi alipoachwa na Chelsea kuliondoa kelele za wadau ambao, walitamani kuomuoa akivaa jezi ya Taifa Stars. 
Adam ana wadogo zake watatu ambao ni Roberto (18) na mapacha wawili, Zion na Paolo (13) ambao wapo katika timu za vijana ya Reading. 

Pengine kama Adam angekaza angekuwa mmoja wa mastaa wakubwa pale England kama ilivyo kwa Pogba, ambaye alicheza naye ligi za vijana nchini humo. 
Pogba alikaza na hata pale alipokosa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza cha Manchester United mbele ya Sir Alex Ferguson alikwenda sehemu ambayo ilimpa nafasi na kumfanya kuwa staa mkubwa Ulaya. 

Mfaransa huyo alirejea United kama staa mkubwa na sio mchezaji wa kawaida kutokana na namna alivyokaza kwenye kupigania ndoto zake akiwa Juventus ambako alijifunza vitu vingi kutoka kwa fundi wa Kiitalia, Andrea Pirlo. 
Nditi kama angekaza naye angeweza kufanya mambo makubwa kama staa huyo. 

Adam Nditi bado kijana mdogo ameishia kucheza ndondo London, huku Pogba akioga mapesa Man utd

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post