Akizungumza katika mahojiano maalum na www.eatv.tv, Katibu Mkuu JKT Tanzania, Abdul Nyumba amesema hawakubaliani na maamuzi hayo kwani wamefanya maandalizi yote na wao ndio wenye haki kama wenyeji, lakini wameshtukizwa na kuambiwa sasa watacheza uwanja wa taifa badala ya Mkwakwani mkoani Tanga.
"Kimsingi sisi hatuna matatizo kabisa na klabu ya Yanga isipokuwa bodi ya ligi wanashindwa kuwela wazi haya mambo, walichokuwa wanasema ni kufanya marekebisho katika uwiano wa mechi za nyumbani na ugenini lakini mechi yetu sisi ni mechi ya kiporo, kama Simba walivyocheza na lipuli," amesema Abdul Nyumba.
"Yanga haohao wamekwenda kucheza na Mwadui FC na Kagera Sugar kwahiyo walipaswa kucheza na sisi katika mechi yetu ya kiporo ambayo ilitakiwa ichezwe tarehe 26 lakini bodi ya ligi ikabadilisha na kuweka tarehe 29 huku mechi ikisomeka JKT Tanzania Vs Yanga sasa tunashangaa kupangwa ichezwe taifa," ameongeza.
Aidha Abdul Nyumba amesisitiza kuwa hawatokuwa tayari kucheza mchezo huo katika uwanja wa taifa hadi pale bodi ya ligi itakapothibitisha kuwa mechi hiyo si ya kiporo bali ni ya mzunguko wa pili, itakayosomeka Yanga dhidi ya JKT Tanzania.
JKT Tanzania inashika nafasi ya sita ya msimamo wa ligi kwa alama zake 19 baada ya kushuka dimbani michezo 13 sawa na Mbeya City na Mbao FC zenye alama hizo.