Neymar kumrithi Ronaldo? Hafai” Ndoo ya bafuni haiwekwi maji ya kunywa”


Wakati mawakala wa Sir Alex Fergson walipofika Brazil walikwenda moja kwa moja mpaka Santos kumtazama Neymar. Mwandishi mmoja wa jarida la the Sun Neil Custis aliandika habari yenye kichwa cha habari kwamba “Man United wanapaswa kuharakisha kutoa Milion 38 kwa Neymar”

Santos wakajifanya kwamba wamekataa ofa ya Paundi milioni 38. Tena kwa mchezaji wa miaka 18! Ni kichekesho kwa kweli.

Binafsi niliona kama ni drama za bongo movie tu. Hakukua na ukweli wowote kuhusu Fergie kutoa kiasi kile cha hela kwa mtoto mdogo kama yule tena kwa hulka yake ya tabia mbovu mbovu. Kwanza Neymar alikuwa amesimamiwa na watu kadhaa nyuma yake kitu ambacho Fergie asingekubaliana nacho. Nani asiyejua kwamba Fergie alikuwa hapendi kununua wachezaji ambao mikataba yao inahusisha watu watatu? Si mnakumbuka sakata la Carlos Teves kuondoka United?

Miaka miwili nyuma yake Roman Abramovich Alituma watu wake kumshawishi Neymar kwenda Chelsea akiwa na miaka 18. Waandishi wa fifa walimfuata na kumhoji kulikoni amekataa ofa ya kwenda Chelsea. Neymar akasema sipaswi kuharakia maisha. Ukweli ni kwamba waliokuwa nyuma ya Neymar walikuwa na tamaa, sio baba sio Ribeiro.

Akiwa Santos Neymar aliutesa ulimwengu wa soka kwa vichwa vya habari akiwa ligi ya Brazil. Alikuwa na urefu wa Mita 1.7 pekee na kilo 60 tu. Wakati ule Ronaldo alikuwa na urefu wa 186 cm na kilo 84.6. Wote walikuwa na uwezo wa kuwapita mabeki lakini utofauti wao ulikuwa aina yake ya uchezaji. Na Fergie alihitaji mrithi wa Ronaldo wakati ule. Je kwanini hakumpata? Ni kweli Ferie alikosa Euro 38 kwa mchezaji mwenye kiwango bora vile?

Siamini kama umbo lake ni tatizo sana kama ilivyokuwa mjadala mkubwa mwaka 2012. Wadau wengi wa soka kipindi kile walisema Neymar hafai kwenda United. Ninachokiamini ni kwamba jicho la Ferguson lilikuwa na mwanga mkali kuliko mawazo ya baba yake Neymar aliyeamini mwanaye anathamani ya kiasi kile.

Nikukumbushe tukio rahisi ambalo kila mmoja aliliona. Unakumbuka sakata lake la kuzozana na Edison Cavan kuhusu Mkwaju wa penati? Tatizo hilo hilo aliwahi kusababisha aliponyimwa nafasi ya kupiga tuta kwenye ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Atletico GO akiwa na miaka 18 tu. Ana mdomo mchafu, dharau na kiburi. Akiwa na miaka 18 alianzisha ugomvi mkubwa na vurugu kwenye mchezo dhidi ya Ceara! Ulitegemea kweli Ferguson atoe Euro milion 38?

Real Madrid wanamuuza Ronaldo na wanataka kuziba pengo lake kwa kupitia Neymar. Tumesikia Real wakitajwa sana kumchukua Neymar. Kuna watu wanaamini Neymar alikwenda PSG ili baadae aende Madrid!!!

Wenye mawazo hayo nao wamewalogwa na kipaji cha Neymar kama mashabiki wa Brazil. Wabrazil baada ya Neymar kuumia mchezo wao dhidi ya Colombia 2014, mchezo uliofuata walikwenda kucheza na Ujerumani. Wakijifanya wana huzuni kubwa kwamba Neymar utadhani kuumia kwake Brazil zima imepigwa ma msiba. Tena wakabeba na vijezi vyao wakaingia uwanjani. Mwisho wa siku wakala 7. Msimu huu Neymar kaumia takribani miezi 6, hajapona vizuri wabrazil wote wakajenga nia ya ubingwa chini ya mtu aliyetokea majeruhi. Eti kisa tu De lima aliwahi kufanya hivyo!

Alichowafanyia Wabrazil hakuna zaidi ya kupoteza muda kuanguka anguka ovyo. De lima akajitahid kumtetea kwamba watu walipanga kumchezea rafu. Yaani watu waache kupanga njama za kumuumiza Messi na Ronaldo wapange kumuumiza Neymar? Kwa lipi?

Lakini Wabrazil hao hao kwenye mazoezi wakatuonesha picha ya Neymar akitudhihaki kuwa amechezewa rafu mazoezini huku akina Coutinho wakimpigia makofi! Utagundua utoto wa kijinga ndio uliangamiza kambi yao.

Wadau wakajiuliza mbona mechi na ubelgiji hizo drama hakuonesha??

Real Madrid wakijichanganya basi wasihangaike kumtafuta mchawi, mchawi ni kipaji cha Neymar. Neymar ana kipaji kuliko mchezaji yoyote hapa duniani kwa sasa. Na kipaji hiki kinafanya watu wamnyenyekee. Lakini hajui akitumieje kwa manufaa yake. Amebaki kuwa Neymarketing.

Ni Neymar huyu huyu akiwa na miaka 17 alimrushia kocha wake jezi kwa hasira. Wala hakuna aliyefungua mdomo kwamba achukuliwe hatua. Wala Wabrazil hawakujali. Ndio hao hao ambao hivi juzi mmiliki mmoja wa Bar kule Rio alitoa ofa ya bia bure kila mara Neymar alipofunga bao katika kombe la dunia.

Ni Neymar huyu huyu Raisi wa PSG aliyeingia kati suala la lake na Cavani. Unadhani Unai alipenda kuondoka PSG? Ukiuliza sababu ni ipi mwisho wa siku utagundua kwamba Neymar amezaliwa hivyo. Kipaji chake ndio uchawi. Yaani ni sawa na mwanamke awe na kalio kubwa. Watu hawatajali sana kuhusu tabia zake mbovu wala akili ila watu watamgeukia kila akipita . Bila shaka kuna mchawi alikuwa anatembea nyuma ya Neymar. Wengi walilogwa.

Kuna wale walioamini Neymar alipaswa kuja Afrika Kusini na Brazil wakati wa kombe la dunia mwaka 2010. Kuna baadhi ya mashabiki akiwemo mwendesha langalanga Felipe Messa walimshurutisha Kocha Dunga kumchukua Neymar akiwa na miaka 18 tu. Watu wakaanzisha kampeni ya kulazimisha Neymar aitwe. Dunga akasema hawezi kwenda nae. Wadau wengi wa soka Brazil walimjia juu sana Dunga hata Dunga alipofi Wabrazil wote wakambwagia Dunga mzigo. kigezo kwanini amwache Neymar.

Kombe la dunia lilipokamilika hapa ndipo tukagundua sura halisi ya Neymar. Klabu yake ya Santos ikamtimua kocha wao Dorival Junior baada ya kocha huyo kumsimamisha Neymar kucheza dabi yao na Corinthians kwa utovu wa nidhamu. Ilipatikana tuta baada ya Neymar kuchewa faulo. Kocha akasema Marcel akapige na wakati huo Neymar alishakimbilia mpira ili apige. Neymar alikerwa sana na kitendo kile na alimfuata kocha na kumtukana matusi machafu. Kitendo kile kilifanya kibarua chake kiote nyasi. Mchezo uliofuata Juniour alimweleza Neymar hatocheza kwenye dabi. Bodi ya Santos ilikasirishwa na kitendo kile na Raisi wa timu Pedro Luis Nunes Conceição alimtimua kocha yule.

Hata hivyo kuna Wabrazil wanajoelewa hasa hasa Mzee Menezes. Mzee Menezes yeye hakulogwa na kipaji cha Neymar. Kocha mkuu wa Brazil Mano Menezes nae aliamua kumtema Neymar kwenye kikosi chake kwa tabia mbaya licha ya kwamba Neymar kufunga katika mchezo wake wa kwanza kabisa kwa taifa hilo kwenye ushindi wa 2-0 dhidi USA.

René Simões mwaka ule ule 2010 aliwambia Wabrazil wenzake kwamba tunatengeneza mnyonya damu tusije kujilaumu hapo baadae. Hakupendezwa kabisa na kitendo cha Neymar kumdharau kocha wake. Ujinga wa kupindukia ni ule tuliouona kule kwenye tuzo za mchezaji bora wa Ufaransa. Eti Neymar akatwaa tuzo ya mchezaji bora! Kwa lipi! Ni kioja.

Naitwa Privaldinho (Instagram) sijamaliza. Nitaendelea. 

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post