Yanga wavamia nyumbani kwa Manji


YANGA hawataki kusikia neno kujiuzulu na sasa wameanzisha mkakati maalumu kuhakikisha Mwenyekiti wao, Yusuf Manji, anarejea kazini.

Taarifa ambazo Mwanasposti imeelezwa ni kuwa wanachama kwa kauli moja wamekubaliana hawakubali Manji kujiuzulu kabisa.

Sasa iko hivi. Baada ya juzi kumaliza mkutano wao pale Bwalo la Maofisa wa Polisi Oysterbay, Dar es Salaam, wakakajikusanya ndani ya daladala mbili na kwenda nyumbani kwa bilionea huyo wakitaka kumuona na kumfikishia ujumbe huo.

Hata hivyo, mpango wao huo haukuweza kufanikiwa na sasa mabosi wa Yanga wanajipanga kutua kwa Manji na kuweka naye mambo sawa.

Mpango mzima ulianza hivi. Juzi Jumapili baada ya kumalizika kwa mkutano huo gari mbili aina ya Toyota Coaster ziliwasili nyumbani kwa Manji saa 10:13 jioni wakitaka kumuona bilionea huyo na kufikisha salamu zao.

Wanachama hao waliona ni kama uongozi wao unachelewa kumrudisha Manji wakiona bosi huyo ndiye mtu pekee anayeweza kuwatoa katika msongo wa mawazo wakati huu watani wao Simba wakitamba kwa kusajili na maisha ya ushindi.

Wakiwa hapo kiu yao iligonga mwamba baada ya mlinzi wa Manji kuwapiga chenga ya maana akiwaambia bosi wake hayupo, lakini atafikisha salamu zao kuwa walikuja.

Hata hivyo, wanachama hao hawakuondoka hivihivi bali waliacha ujumbe mzito wakimwambia mlinzi huyo ambaye hakutaka hata kuwapa upenyo wa kuchungulia ndani ya nyumba hiyo, afikishe salamu kwa Manji kuwa watarudi siku nyingine.

Uongozi utamfuata

Jana Jumatatu Mwanaspoti lilifanya mahojiano na Kaimu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga, aliyeongoza mkutano wa juzi ambaye amesema watawasiliana na Manji kwani, bado ni Mwenyekiti wa klabu na wanachama wanafahamu hilo.

Sanga amesisitiza hana tatizo na kurudi kwa Manji klabuni hapo, alisema hatua ya kumfuata bosi wake huyo inatokana na maamuzi ya mwisho ya klabu ambayo yametoka katika mkutano mkuu halali na kupitishwa kuwa wanachama hawatambui kujiuzulu kwake.

“Unajua kama nilivyosema katika mkutano bahati mbaya nyie waandishi hamkuwepo, lakini naamini mtakuwa mmesikia, maamuzi ya Manji kujiuzulu hayakupata baraka zozote ndani ya klabu yetu,” alisema Sanga.

“Viongozi wa matawi walipinga maamuzi hayo, ikafuata Kamati ya Utendaji nayo ikagoma kukubaliana na hilo, hata Baraza la Wadhamini nalo lilipinga, lakini pia walimfuata na kuzungumza naye.

“Hatua ya mwisho ilikuwa ni jana (juzi) kwa wanachama kuhojiwa kwa nafasi yao wanalionaje hilo na wao wakasema hawakubaliani bado wanamtambua kuwa Mwenyekiti wao sasa kitakachofuata hapo tutamtafuta Manji na kumwambia kwamba bado ni Mwenyekiti.

“Muda bado upo kwa kuwa tumepewa muda maalum wa kutengeneza uongozi wetu na nitaongoza hiyo kazi kuhakikisha tunampata ili tumfikishie huo ujumbe pia tutamwandikia msimamo huo wa wanachama.”

KAMATI YA watu 12

Katika sintofahamu ya kamati mpya iliyoundwa kuhakikisha inatafuta fedha na kufanya usajili, Sanga alisema kamati hiyo haitafanya usajili kwa kuwa hilo si jukumu lao.

Sanga alisema kamati hiyo itakayongozwa na Mwenyekiti Tarimba Abbas akisaidiwa na Said Meck Sadiq, jukumu lake kubwa litakuwa ni kutafuta fedha zitakazosaidia kutengeneza kikosi hicho, lakini majukumu ya kusajili yatabaki kwa Kamati ya Usajili iliyo chini ya Mwenyekiti wake, Hussein Nyika ambayo haijavunjwa.

Alisema wiki hii atakutana na kamati zote lengo likiwa kuwapa miongozo ya kamati zao waweze kushirikiana kuleta mafanikio yaliyokusudiwa.

“Kuna kitu hakijaeleweka kwenu, kamati tuliyoiunda haina jukumu la kufanya majukumu ya usajili hapa naomba tuelewane tusichanganye mambo, kamati hii kazi yake ni kutafuta fedha ili zitumike kutengeneza timu,” alisema Sanga

“Kazi ya kusajili itabaki kama ilivyokuwa chini ya kamati ya usajili kutokana na kamati ya usajili inatakiwa kuundwa na kuongozwa na wajumbe wa kamati ya utendaji kwa mujibu wa katiba, sasa kama utaona wanaoongoza ile kamati sio wajumbe wa kamati ya utendaji.”

“Nimepanga kukutana na kamati zote ikiwezekana wiki hii ili kuweza kuzungumza nao na kuwapa miongozo.”

SOURCE: MWANASPOTI

Post a Comment

Kwa maoni na ushauri weka comment yako hapo chini:

Previous Post Next Post